NGOs ZAASWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA TAIFA
Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameyatahadharisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya Taifa na kujiepusha na harakati zozote zinazokinzana na mila na desturi za kitanzania.
Kanali Thomas ametoa tahadhari hiyo wakati anafungua mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Ruvuma uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
“Jiepusheni na kuchochea mahusiano ya jinsia moja,mkifanya hivyo serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa shirika lolote lisilo la kiserikali litakaloshindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria,kanuni na miongozo’’,alisema Kanali Thomas.
Amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa na serikali bila kujali mchango unaotolewa na shirika hilo katika kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameyataja mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuwa yanachangia maendeleo makubwa ndani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla na kwamba serikali inatambua mchango huo ndiyo maana imeweka sera na sheria ili kuhakikisha NGOs zinafanya kazi kwa kuzingatia sera,sheria na miongozo.
Ameyaonya baadhi ya mashirika ambayo yanafanya kazi bila kuzingatia miongozo ambapo amesema yanajiweka katika hatari ya kufutwa katika orodha ya NGOs nchini.
Awali Mratibu na Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Ruvuma Xsaveria Mlimira akitoa taarifa ya NGOs katika Mkoa amesema hadi sasa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya NGSs 166 baada ya uhakiki ambao ulifanyika mwaka 2022.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma kuna mashirika nane kutoka nje ya nchi ambayo yanashiriki katika shughuli za maendeleo kwenye sekta za afya,elimu na kilimo.
Ameyataja baadhi ya mafanikio ya NGOs mkoani Ruvuma kuwa ni kutoa mafunzo kwa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya,kusaidia gharama za kufanya usimamizi shirikishi katika eneo la ukoma na kifua kikuu na kuchochea mahudhurio ya akinamama kujifungua yameongezeka kutoka asilimia 94 hadi 99 mwaka 2022.
Mafanikio ya NGOs katika sekta ya kilimo ameyataja kuwa ni kukua kwa mitaji ya wakulima wadogo 10,000 toka shilingi milioni 80 mwaka 2019/2020 hadi kufikia shilingi bilioni 6.3 mwaka 2022/2023.
Katika mkutano huo mada mbalimbali zilitolewa zikiwemo sheria za mikataba,uandikishaji na uendeshaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kampeni ya Mama Samia ya kutoa msaada wa kisheria kwa jamii ambayo inatarajiwa kuzinduliwa Julai 22,2023 mkoani Ruvuma.Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza wakati anafungua mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nmkoani Ruvuma,uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kushirikisha NGOs 166 zinazofanya kazi mkoani RuvumaBaadhi ya wadau wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali NGOs wakiwa kwenye mkutano wa mwaka wa mashirika hayo mkoani Ruvuma uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.Mkoa wa Ruvuma una NGOs 166 baada ya uhakiki uliofanyika mwaka 2022.
Post a Comment