Header Ads

test

SERIKALI YARIDHIA WAKULIMA RUVUMA KUENDELEA KUUZA MAZAO KWENYE MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Na Albano Midelo,Tunduru

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeridhia wakulima kuendelea kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kanali Thomas amesemayo hayo mjini Tunduru wakati anazungumza na viongozi na watendaji wa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma katika majumuisho ya vikao maalum vya mabaraza ya madiwani ya kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
vilivyofanyika kila Halmashauri kuanzia Juni 19 hadi 26,2023.

“Kupitia kikao hiki napenda kuwajulisha kuwa Waziri wa Kilimo ameandika barua ya kuridhia mfumo wa stakabadhi ghalani kuendelea kutumika katika Mkoa wa Ruvuma kutokana na mafanikio makubwa yanayopatikana kwa wakulima na Halmashauri kutokana na kuuza mazao kupitia mfumo
huo’’,alisisitiza Kanali Thomas.

Amesema wakulima mkoani Ruvuma wameweza kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 87 baada ya kuuza mazao ya ufuta,soya,mbaazi,korosho na kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Hata hivyo amesema wanaopinga mfumo huo sio wakulima bali ni watu
wa kati wakiwemo wafanyabiashara na baadhi ya watumishi na madiwani katika Halmashauri ya Tunduru wanaotorosha mazao na Kwenda kuyauza nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani nje ya Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Komredi Oddo Mwisho akizungumza kwenye kikao hicho ameutaja mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa upo kwenye Ilani ya CCM hivyo unatakiwa kutumika kuuza mazao ya wakulima ili kutoa tija baada ya
wakulima kuuza mazao bei ya ushindani.

“Mfumo wa stakabadhi ghalani ni matakwa ya Ilani ya CCM,kipengele cha 34(i) kinazungumzia wakulima kuuza mazao ya stakabadhi ghalani,pia umetolewa mwongozo wa mazao yanayotakiwa kuuzwa kwenye mfumohuu”,amesisitiza Komred Mwisho.

Amesisitiza kuwa wakulima kuendelea kuuza mazao yao kupitia mfumo huo ni kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo hivyo wakulima kufaidika badala ya kunyonywa na mfumo holela.

Amewatahadharisha wasiruhusiwe wafanyabiashara au mtu yeyote anayetaka kukwamisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao ni wa wakulima pekee.

Amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 itahakikisha inasimamia mfumo wa stakabadhi ghalani na kutafuta masoko bora ya wakulima.

Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja amezitaja faida za Mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa ni Pamoja na wakulima kukutanishwa na wanunuzi hivyo kuwafanya wawe na maamuzi ya kuuza mazao yao kwa umoja wao na kuwepo kwa matumizi ya vipimo halali vya wakulima kwa sababu wanunuzi hutumia mizani iliyohakikiwa na wakala wa vipimo.

Amezitaja faida nyingine za mfumo huo kuwa ni upatikanaji wa tozo za serikali kwa njia rahisi,kuongezeka kwa bei ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi ambao umetokana na kuongezeka kwa wanunuzi ambao wanashindanishwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kutoa bei kubwa kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza na viongozi na watendaji kutoka Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kwenye kikao cha majumuisho ya CAG kilichofanyika kwenye ukumbi wa Skyway mjini Tunduru pamoja na mambo mengine alieleza namna serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilivyoridhia wakulima katika Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred Oddo Mwisho akizungumza kwenye kikao cha majumuisho  ya CAG kwenye ukumbi wa Skyway mjini Tunduru.

Baadhi ya waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwenye kikao cha majumisho ya CAG mjini Tunduru.

No comments