Header Ads

test

TAARIFA YA UKUSANYAJI MAPATO YATAWALA BARAZA LA MADIWANI NAMTUMBO.

Kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma lilitawaliwa na majadiliano ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri yao.

Akichangia kwenye kikao cha baraza hilo diwani wa kata ya Mkongo Daniel Nyambo alisema Hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo inahitajika jitihada za ziada na kuongeza ushirikiano wa pamoja kati ya wataalamu na waheshimiwa madiwani .

Nyambo alidai licha ya Halmashauri hiyo kujipatia mapato kupitia ushuru utokanao na mauzo ya mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani bado kuna mianya ya utoroshaji wa mazao ambayo hayapo katika mfumo wa mauzo ya stakabadhi ghalani hivyo alitaka wataalamu na waheshimiwa madiwani kuongeza ushirikiano ili kudhibiti mianya ya utoroshaji wa ushuru wa mazao na kuikosesha Halmashauri mapato yake.

Sambode Mhongo Diwani wa kata ya Ligera aliwataka watendaji wa kata waliopewa mashine za kukusanyia mapato kusimamiwa ipasavyo kwani alidai wapo wanaokusanya na kubaki na fedha bila kupeleka benki na wengine kujikopesha.

Mhongo pamoja na kusema hayo alisisitiza Halmashauri kuwashughulikia watendaji wanaotumia fedha walizozikusanya kwa shughuli zao binafsi.

Naye Paul Fusi diwani wa kata ya Litola pamoja na mambo mengine alihimiza wakusanya mapato magetini walipwe posho zao ili wafanye kazi ya kukusanya fedha bila kuwa na malalamiko ya kutolipwa posho zao.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Chiriku Hamis Chilumba pamoja na kuwashukuru waheshimiwa madiwani kwa kuonesha msisitizo katika ukusanyaji wa mapato aliwaambia waheshimiwa madiwani kuwa inatakiwa kuunganisha nguvu katika swala la ukusanyaji mapato.

Chilumba alidai ofisi yake imewataka watendaji wa kata wenye madeni kutoka kwenye mashine za ukusanyaji mapato kulipa madeni hayo na baada ya hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Jumma Halfan Pandu alimwagiza mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuendelea kusimamia ukusanyaji mapato ya Halmashauri,kusimamia miradi ya ujenzi ya boost na swash ili iweze kukamilika kwa wakati.

Hassani Bakari Nyange katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo aliyemwakilisha mkuu wa wilaya katika kikao hicho cha baraza la madiwani alidai ofisi ya mkuu wa wilaya imemwandikia barua mkurugenzi mtendaji kuomba majina ya watendaji wa kata wanaodaiwa fedha za serikali .

Aidha Nyange aliwaambia waheshimiwa madiwani kuwa kutumia fedha ya serikali kinyume na taratibu ni kosa kisheria hivyo watendaji waliofanya hivyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Mkutano wa baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kupitia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za kudumu za Halmashauri kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023 limefanyika katika ukumbi wa Halmashauri tarehe 28 mwezi huu na kukubaliana kuongeza kasi ya kuunganisha nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa waheshimiwa madiwani na wataalamu wa Halmashauri hiyo.









No comments