DC SINGIDA : WAFANYABIASHARA VIPODOZI SHIRIKIANENI NA SERIKALI KATIKA KUDHIBITHI VIPODOZI VYENYE SUMU
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, akizungumza na Wafanyabiashara wa Vipodozi Mkoa wa Singida Julai 27, 2023, wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara hao cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu.
.......................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili amewataka
wafanyabiashara wa vipodozi mkoani hapa kushirikiana na Serikali pamoja na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kudhibiti bidhaa zenye viambata vyenye sumu.
Mragili alitoa ombi hilo wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara
cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu Mkoa wa
Singida.
Hatua ya TBS kutoe elimu hiyo ilifuatia maombi yaliyotolewa na
wafanyabiashara hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwezi Mei, 2023 wakati
maafisa wa TBS walipoanzisha operesheni ya kupita katika maduka ya vipodozi kwa
lengo ya kuondoa bidhaa hizo katika soko ambazo zinaathari kwa binadamu.
“Mwezi Mei mliniletea malalamiko kuwa maafisa wa TBS wamefika kwenye maduka
yenu na kuanza kuondoa vipodozi ambavyo havikubaliki kwa matumizi ya binadamu
mkidai operesheni hiyo ilikuwa ikifanyika bila ya kupewa uelewa wa matumizi ya
bidhaa hizo, niliona mlikuwa na hoja ya msingi licha ya TBS kutangaza jambo
hilo tangu mapema ndipo nilichukua uamuzi wa kuwazuia maafisa hao ili mpate
mafunzo hayo na twende pamoja,´alisema Mragili.
Alisema anawapongeza sana TBS kwani baada ya kuwazuia kutokana na uungwana
wao licha ya kuwa walikuwa wakitekeleza wajibu wao kisheria Mwezi Juni
2023 walirudi tena Singida na kufanya kikao na wafanyabiashara hao na kuwapa
elimu na sasa wamerudi tena kwa mara nyingine kwa lengo lilelile.
Alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndio limepewa
jukumu la kusimamia vipodozi hivyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya
Mwaka 2019 ambapo limekuja na mkakati wa
kuelimisha wananchi juu aina ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa
marufuku kwenye soko la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendesha ukaguzi wa
kushtukiza kwenye soko kwa lengo la kuviondoa , kutoa elimu kwa umma na kuvisajili.
Mragili alisema kuendelea kuviuza na kuvitumia vipodozi
hivyo ni hatari kwani wanaliangamiza taifa jambo ambalo ni hatari na
halikubaliki na kwamba baada ya mafunzo hayo hategemei kuona bidhaa hizo
zikiendelea kuwepo kwenye soko ambapo alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara hao
kuviondoa mara moja kabla havijakutwa na maafisa wa TBS na kuvikamata.
“ Baada ya mafunzo haya hatutakuwa na huruma na
mfanyabiashara yeyote atakayekamatwa akiendelea kuwa na vipodozi hivyo kwenye
soko na hasije akatuambia ni bahati mbaya ninyi mnamtandao mkubwa nendeni
mkawaambie na wenzenu kwani wanaoathirika navyo si wale tu mnaowauzia bali na
ndugu zenu pia,” alisema Mragili.
Aliwataka wafanyabiashara hao waache kuangalia
upande mmoja tu wa kuwa watakosa fedha bali wawe na dhamira ya kulinda afya za
watanzania.
Awali akitoa mafunzo hayo Meneja wa TBS Kanda ya
Kati, Nickonia Mwabuka alisema matumizi ya vipodozi hivyo vyenye viambata
vyenye sumu ni hatari kwa afya ya binadamu na vimekuwa vikiwaathiri watu wengi
na kuliongezea taifa gharama kubwa ya kuwatibu waathirika na kupunguza nguvu
kazi ya taifa.
Alivitaja vipodozi visivyo salama ni vile ambavyo vina kemikali zinazoweza
kuudhuru mwili na kuusababishia matatizo, ambavyo havijasajiliwa na TBS, vipodozi
vyenye viambata (kemikali) vya sumu na vilivyopigwa marufuku, ambavyo muda wake
wa matumizi umeisha, vipodozi ambavyo havioneshi tarehe ya kuharibika (Expire-date).
Vingine ni vile ambavyo maelezo yake hayajaandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza
ambavyo vinaweza vikawa ni mafuta, losheni, krimu, pafyumu, poda na kadhalika.
Mwabuka alitumia nafasi hiyo kuwataka
wafanyabiashara wa vipodozi hivyo kupeleka taarifa za vipodozi wanavyouza ikiwa
ni pamoja na kuvisajili kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wake., hatua
itakayowasaidia kujua ni vipodozi vipi vimepigwa marufuku na vile
vinavyoruhusiwa kwenye soko la Tanzania.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wauzaji wa Vipodozi Mkoa
wa Singida, Pili Hussein akizungumza kwa niaba ya wenzake aliomba Serikali
kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa wa bidhaa hizo ambao wamekuwa wakiwauzia.
“Tunashindwa kuelewa kuna vyombo husika vya ukaguzi katika bandari, viwanja vya Ndege na mipakani ambako bidhaa hizi zinapitishwa na wafanyabiashara wakubwa na kusajiliwa ambao wanafahamika lakini wanaacha kuwadhibiti hadi zikifika kwetu ndio wanakuja kuzikamata jambo hili sio zuri kwani linaturudisha nyuma na kufilisi mitaji yetu,” alisema Hussein.
Post a Comment