DK.MWIGULU ATAKA TAKWIMU SAHIHI ZITUMIKE KUPANGA MIPANGO YA MAENDELEO, AWAOMBA WATANZANIA KUMUOMBEA RAIS SAMIA
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, akihutubia wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Singida yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Kizaga wilayani Iramba Julai 1, 2023.
..................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa
serikali kuzingatia matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi
katika Mipango ya Maendeleo.
Nchemba ameyasema hayo mkoani Singida jana wakati akifungua mafunzo ya
usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa
viongozi na watendaji wa Mkoa wa Singida yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya
Kizaga wilayani Iramba.
Alisema mipango mingi inashindwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na
kutokutumia Takwimu zilizopo katika kupanga mipango hiyo kwenye shughuli
mbalimbali.
“Tuzingatie Takwimu sahihi zilizopo, matokeo ya Takwimu na maoteo
itatusaidia sana uko mbele tuendako kwani zamani sensa ililenga zaidi kujua
idadi ya watu,” alisema Mwigulu.
Akitoa mfano mdogo wa kutofanya mambo yetu kwa Takwimu alisema inakuweje
inatokea tuna walimu wengi wa baadhi ya masomo hawana hata nafasi, lakini
kwenye nchi hiyo hiyo kuna walimu wengi
ambao akili zinalingana na hawana masomo.
Dk. Mwigulu alisema kutozingatia Takwimu tumekuwa na dharura nyingi ambazo
zimekuwa zikiipa nchi changamoto kubwa akitolea mfano wa Serikali ilipolazimika
kujenga shule za sekondari za kata nchi nzima kufuatia kuwepo na wanafunzi
wengi waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza kushindwa kupelekwa shuleni kwa
kukosa mahali pa kusoma.
Alisema mambo hayo ya dharura na kutozingatia takwimu yamekuwa yakimpa Rais
wakati mgumu akitoa mfano kuwa leo anapelekewa idadi ya ujenzi wa madarasa pengine 100, anayajenga na baada
ya siku chache anaambiwa tena idadi ile haikuwa sawasawa hivyo madarasa hayo
hayatoshi.
Awali kabla ya kufungua mafunzo hayo Dk.Mwigulu aliwaomba watanzania
kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu
Hassan kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi
ambapo kwa muda mfupi aliokaa madarakani ameweza kufanya mambo makubwa ambayo
yamemgusa kila mtanzania.
Akitaja baadhi ya mambo hayo ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao
ujenzi wake umebakia asilimia 15 ukamilike, ujenzi wa zahanati na vituo vya
afya nchi nzima, kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za vijijini (TARURA)
kutoka Sh.Bilioni 200 hadi kufikia Sh. Trioni 1, kuongeza bajeti ya kilimo
kutoka Sh.Bilioni 200 hadi kufikia Trioni moja na Bilioni 200 bajeti ambayo
haijawa kufikiwa na awamu zote za Serikali zilizopita.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
kutoka Bilioni 400 hadi kufikia Bilioni 750 na kuviingiza kwenye mikopo vyuo
vya kati vya afya , elimu na vya ufundi zaidi ya 50 sanjari na kutoa elimu bure
kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.
Dk.Mwigulu alitumia nafasi hiyo kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) chini
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya
kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya kukamilisha mipango ya maendeleo nchini.
Aidha, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kwa kazi kubwa
anayoifanya ya kuhamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo na kuifuatilia
kwa karibu.
“Hii ni faida kubwa ya kuwa na mkuu wa mkoa ambaye aliwahi kuwa mbunge
mwenye uwezo wa kujua mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi anatusaidia hata
sisi wabunge wa mkoa huu katika maeneo mbalimbali endeleeni kumpatia ushirikiano,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alisema Mipango na programu zote za maendeleo za mkoa huo
zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa hiyo ya Watu na Makazi, Majengo na
Sensa ya Anuani za Makazi ya mwaka 2020/
2022.
Alisema katika mipango na programu za mwaka wa fedha 2023/2024
zimezingatia matokeo ya Sensa na takwimu nyingine zinazozalishwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na kuwa ili wananchi wa
mkoa wa Singida waweze kupata huduma Bora, mipango ya mkoa huo itazingatia matumizi ya matokeo ya sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Mtakwimu Mwandamizi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu- (NBS), Mdoka Omary alisema
madhumini ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo ya sensa ya watu na makazi
ya mwaka 2020/ 2022 na kuwajengea uwezo
wadau wote na viongozi namna ya kutumia matokeo
hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na utendaji katika Serikali kuu
na mamlaka ya Serikali za mitaa.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uwezo na kupanua wigo wa matumizi ya sensa ya watu na makazi kwa Serikali.
Post a Comment