TTCL YAWESHESHA SHUGHULI UPANDAJI MLIMA KILIMANJARO KUONEKANA 'LIVE' SABASABA
Baadhi ya wateja waliotembelea Banda la TTCL kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa wakipata huduma zinazotolewa na shirika hilo katika viwanja vya Sabasaba. |
Na Joachim Mushi, Dar
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) limewezesha shughuli za upandaji Mlima Kilimanjaro zinazoendelea hivi sasa muda wote kuonekana moja kwa moja katika viwanja vya Sabasaba ndani ya Banda la TTCL kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Unapokuwa ndani ya Banda la TTCL katika Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa utashuhudia 'live' watalii wanaopanda na kushuka kwenye Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza ndani ya Banda la TTCL Corporation Afisa Uhusiano wa TTCL, Ester Mbanguka alisema miongoni mwa bidhaa ambazo Shirika hilo limeileta katika Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa mwaka huu ni intaneti yenye kasi zaidi (Public Wifi) ambayo inawezesha kuonekana moja kwa moja kwa shughuli za upandani Mlima Kilimanjaro moja kwa moja ndani ya Banda la TTCL.
"..Mteja anayekuja kutembelea Banda la TTCL viwanja vya Sabasaba anapata fursa ya kushuhudia moja kwa moja shughuli za upandaji Mlima Kilimanjaro, unawaona watalii wakipanda na kushuka mlima moja kwa moja hii yote inawezeshwa na huduma mawasiliano ya intaneti yenye kasi zaidi ya inayotolewa na TTCL katika maeneo ya wazi ikiwepo Mlima Kilimanjaro alisema Afisa Uhusiano wa TTCL, Ester Mbanguka akizungumza na mwandishi wa habari.
Alisema miongoni mwa bidhaa nyingine ambazo TTCL Corporation imewaletea wananchi katika Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa ni pamoja na huduma za Faiba Mlangoni Kwako, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huduma za Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data kimtandao 'NIDC' na Huduma za 'Wifi' bure katika eneo la TTCL Viwanja vya Sabasaba.
Aidha aliwataka Wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba mwaka huu kupita katika Banda la TTCL kwa ajili ya kupata Elimu na taarifa zaidi namna ya kufurahia huduma ya intaneti yenye kasi zaidi inavyoweza kuchangia Taifa na wananchi kukua na kunufaika na Uchumi wa kidijitali.
'...Msimu huu tumekuja kuwaonesha Wateja wetu mageuzi makubwa ya Mawasiliano,tulipotoka,tulipo na tunafungua milango ya Uchumi wa Kidijitali.Hivyo tunawaalika sana waje wajionee mambo makubwa yanayofanywa na TTCL katika suala zima la Mawasiliano ya uhakika.
Zaidi ya mataifa 30 duniani yanashiriki katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa Wilaya ya Temeke. Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na China, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uturuki, Kenya, Ghana, India, Singapore, Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Indonesia, Rwanda, Algeria na Pakistan.
Kauli mbiu ya Maonesho ya Sabasaba kwa Mwaka huu ni Tanzania Mahali sahihi kwa Biashara na Uwekezaji.
Post a Comment