Header Ads

test

BIASHARA KATI YA CHINA, TANZANIA YAONGEZEKA

Na Selemani Msuya

BALOZI wa China nchini, Chen Mingjian, amesema ukuaji wa biashara kati yake Tanzania kuanzia mwaka 2022 hadi Juni, 2023, umefikia Dola za Marekani bilioni 8.31 sawa na shilingi trilioni 20 za Kitanzania, ikiwa ni zaidi ya mara tatu na nusu ya muongo uliopita.

Aidha mataifa hayo yamezidi kuimarisha uhusiano ndani ya miaka 10 ya kutekelezwa kwa Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), unaoratibiwa na China ambao umefungua fursa nyingi za biashara baina ya wananchi wa mataifa hayo.

Balozi wa China nchini, Mingjian amesema hivi karibuni wakati wa kongamano la miaka 10 ya kutekelezwa kwa mpango wa BRI ambapo zaidi ya watu 180 wameshiriki.

Alisema manufaa ya BRI nchini, yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara ya nchi hizo hivyo ni imani yake kubwa mafanikio yataongezeka.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa 52 ya Afrika yaliyoridhia BRI ambayo inatimiza miaka 10 hasa kwenye ujenzi wa miundombinu muhimu katika kuchochea maendeleo.

Balozi Mingjian alisema uhusiano baina ya Tanzania na China ndani ya miaka 10 sasa ya kutekelezwa kwa mpango wa BRI umezidi kuimarika na kujengeka ambapo biashara baina yetu na imefikia Dola za Marekani bilioni 8.31,hii ni ukuaji wa wa zaidi ya maratatu na nusu ukilinganisha na kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alisema bidhaa za Tanzania zilizoingia kwenye soko la China zimeongezeka ikiwemo soya, parachichi na nyingine nyingi zimeshaingia kwenye soko hilo na zinaendelea kufanya vizuri.

Alisema kupitia mpango wa BRI, uwekezaji wa China nchini Tanzania umeongezeka ambapo sasa taifa hilo ndilo linaongoza kwa uwekezaji wa miradi mikubwa ikiwa ni mara mbili na nusu ya miaka 10 iliyopita.

"Miradi mikubwa ya maendeleo mfano ya ujenzi wa reli ya kisasa nchini Tanzania vinatekelezwa na kampuni za China ikiwemo ya Reli ya SRG, Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (NJHPP), Bomba la Mafuta kutoka Uganda kuelekea Tanga, Mkongo wa Taifa na miradi mingine mikubwa,"alisema.

Alisema pia Tanzania imenufaika na fursa za ufadhili wa masomo ambapo zaidi ya wanafunzi 2,000 wa Kitanzania wamenufaika nazo huku pia taifa likinufaika na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vilivyojengwa kwenye maeneo tofauti nchini.

Aidha, alisema maktaba kuu ya UDSM, imejengwa kwa ufadhili wa watu wa China na kuwa fursa nyingine lukuki zimetolewa kwa Watanzania vijana kuongeza ujuzi na maarifa katika maendeleo ya teknolojia na hiyo ni matokeo chanya ya kutekelezwa kwa mpango wa BRI nchini.

Akifungua kongamano hilo, Naibu Spika wa Tanzania Mussa Hassan alisema Mpango wa BRI kwa Tanzania umefungua fursa nyingi za maendeleo na kuimarisha zaidi uhusiano baina ya Tanzania na China.

Alisema China imeendelea kuwa rafiki na mdau muhimu wa maendeleo kwa mataifa ya Afrika hususan katika kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa kama ya ujenzi wa miundombinu na hiyo imesaidia kuunganisha mataifa ya Afrika zikiwemo nchi za Afrika Mashariki kwa barabara za lami.

Zungu alisema ushirikiano wa Tanzania na China unapaswa kuendelezwa kwa kuwa una lengo la kuchochea maendeleo na sio manufaa ya upande mmoja.

"China ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Tanzania, hivyo tunapaswa kutumia BRI kuhakikisha tunafika huko ilipo kwani ni wazi mpango huu una faida kwa jamii zetu sisi wa nchi zinazoendelea,"alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku akizungumza kwenye kongamano hilo alisema Tanzania na nchi za Afrika zimenufaika na mpango wa BRI katika eneo la amani, umoja na maendeleo.

Alisema mpango huo ambao umesaidia kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu mikubwa ya ujenzi kama ya reli ya kisasa ambazo zitaunganisha mataifa ya Afrika Mashariki.

“Taasisi ya Mwalimu Nyerere tunaridhishwa na ushirikiano baina ya China na Tanzania, wamekuwa rafiki wakubwa kwa taifa letu, tangu enzi za kiongozi wa taifa hilo Mao Zedong na Mwalimu Nyerere hadi leo, naamini tukiamua kuitumia BRI kama Wachina wanavyotaka tutafika mbali,”alisema Butiku.

Mwenyekiti huyo alisema Afrika inapaswa kuitumia China kwa usahihi kwa kuwa inataka nchi zote kuendelea kwa pamoja na sio kunyonya kama zingine zinavyofanya.

"China inatamani nchi kuendelea sio kutawala wengine, wao wanatafuta ushirikiano na kufanya biashara ni masuala ya amani,umoja na maendeleo,"alisema.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard Kasesera amewataka Watanzania kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana China kwa faida.

"China inahitaji mazao mbalimbali kutoka Tanzania kama Muhogo na mengine, nadhani tunapaswa kulima kwa nguvu zote ili tuweze kunufaika na soko hilo,"alisema.

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara Muttamwega Mgaywa alisema Tanzania inapaswa kukuza na kuendeleza ujuzi ambao unapatikana China ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa unafanyika hapa nchini.

Mgaywa alisema mafanikio ya China yamechangiwa na uthubutu, hivyo ni jukumu la Tanzania na nchi za Afrika kuishi mfano huo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mstaafu, Profesa Anna Tibaijuka alisema BRI ni njia sahihi ya kuzifanya nchi za Afrika kufikia malengo, hivyo ni jukumu la viongozi kuisimamia kwa nguvu kubwa.

Mpango wa BRI ulianzishwa China mwaka 2013 kusaidia mataifa mbalimbali katika bara la Asia, Afrika na Ulaya ambapo zaidi ya nchi 150 zimenufaika na uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani trilioni moja, huku miradi mbalimbali ya ushirikiano 3,000 ikitekelezwa na ajira zaidi ya 420,000 zikitolewa katika nchi zilizojiunga na mpango huo.

Aidha mpango huo umesaidia takribani watu milioni 40 kuondoka kwenye umaskini uliokithiri katika mataifa hayo yaliyojiunga na BRI.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu akifungua kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BRI.
Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BR.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku akizungumza kwenye kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BRI.

No comments