Header Ads

test

DIB YAWAOMBA WATEJA WALIO KATIKA BENKI ZILIZO CHINI YA UFILISI KUFUATA FIDIA ZAO

BODI Ya Bima ya Amana (DIB,) imetoa wito kwa wateja mbalimbali walio katika Benki zilizo chini ya ufilisi kufuata fidia zao za bima ya Amana, fedha ambazo bado hazijachukuliwa na baadhi ya wateja kutoka kwa benki zilizoanguka.

Akizungumza wakati akizindua warsha ya siku mbili kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini leo jijini Dar es Salaam; Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB,) Isaac Kihwili amesema kiwango cha bima ya amana ya shilingi milioni 1.5 kwa baadhi ya wateja hakijachukuliwa licha ya kufanya jitihada mbalimbali za kuwatafuta.

"Tumejaribu kuwatafuta kupitia namba zao za simu, taarifa katika mafaili yao katika mabenki pamoja na kutumia fursa za matangazo katika maonesho ya Sabasaba na NaneNane, vyombo vya habari na Tovuti ya Taasisi, Fedha zao zipo tunaomba waje wazichukue." Amesema.

Kuhusiana na kiwango cha bima ya amana, Kihwili ameeleza kuwa kwa kiwango hicho kwa sasa ni shilingi milioni 7.5 na awali ilikuwa shilingi milioni 1.5 kuanzia mwaka 2010 na mwaka huu mwezi Machi Serikali ilibadili kiwango hicho ambacho bado hakijaanza kutumika.

"Sababu ya Serikali kubadili kiwango hicho ni pamoja na kupanda kwa thamani ya fedha kutoka milioni 1.5 ya mwaka 2010 hadi kufikia shilingi milioni 7.5, uwezo wa mfuko ambao tumeona unauwezo wa kugharamia kiwango hicho na kikubwa na usikivu wa Serikali kwa malalamiko ya wananchi kuhusiana na uchache wa Amana uliopelekea Serikali kupitia Wizara ya Fedha kutoa maelekezo ya kuangalia namna ya kufanya maboresho hayo ambayo Bodi itamudu kuhudumia baada ya baadhi ya mabenki kuanguka." Amesema.

Amesema, kiwango hicho kipya cha milioni 7.5 hakijaanza kutumika kutokana na kutokuwa na anguko la benki yoyote tangu kiwango hicho kianzishwe na Benki ambazo zipo kwenye ufilisi na wateja wake wanaendelea kulipwa kiwango kitakachotumika ni kile cha zamani na ikitokea benki ikianguka kipindi hiki fidia itakayolipwa ni shilingi milioni 7.5.

Aidha kuhusiana na suala la ufilisi wa benki mbalimbali amesema, kinachoendelea sasa ni ukusanyaji wa Mali za benki hizo ikiwemo samani ambazo huuzwa pamoja na kukusanya mikopo ili walioweka Amana katika benki hizo waweze kulipwa Fedha zao.

"Tumeteua kampuni mbili za udalali zitaanza zoezi la ufuatiliaji wa mikopo hiyo, tunaomba wananchi waliokopa watoe ushirikiano kwa madalali hao na kuondokana na dhana kwamba benki ikianguka basi jukumu la kulipa limeishia hapo, ni dhana potofu tulipe madeni ili walioweka Amana katika benki hizo wapate stahiki zao." Ameeleza.

Kihwili amesema, Bodi hiyo ni taasisi ya Serikali ambayo ina jukumu kutoa bima ya amana kwa ajili ya wateja mbalimbali wa benki kwa amana zilizopo kwa mujibu wa Sheria.

"Bima ya Amana ni utaratibu ambao umeanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuwalinda wateja wa Benki, kimsingi hii ni muhimu kwa kuwa mwananchi au mwenye amana anapokuwa na uhakika wa usalama wa pesa zake basi tunakuwa na uhakika wa utulivu wa sekta ya benki nchini." Amesema.

Amesema, Katika Warsha hiyo ya siku mbili imelenga kuwajengea uwezo Wahariri wa vyombo vya habari na kupitia kwao wananchi waweze kufahamu majukumu ya Bodi hiyo, malengo na umuhimu wa Bodi hiyo kwa Tanzania na ulimwenguni kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB,) Isaac Kihwili akizungumza wakati akizindua warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri wa vyombo vya habari nchini na kutoa wito kwa wateja mbalimbali walio katika Benki zilizo chini ya ufilisi kufuata fidia zao. Leo jijini Dar es Salaam

Afisa Sheria Mwandamizi wa DIB Acley Chaula akitoa mada ya Muktadha wa Bima ya Amana Tanzania katika warsha ya siku mbili iliyoikutanisha Bodi hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari nchini, Leo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi wa Bodi ya Bima ya Amana wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali.


No comments