KIZIMBANI KWA KUISABABISHIA UDA HASARA YA SH.BILIONI 14
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
WAFANYABIASHARA Saimon Bulenganija (43), William Kisena (44) na Leonard Lubuye wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha ya Sh. bilioni 14 na kulisababishia Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) hasara
Mapema, upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa serikali Fatuma Waziri uliiomba mahamama kumfutia mashtaka mshtakiwa Lubuye wakieleza kuwa, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi dhidi yake.
Kufuatia ombi hilo Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi alimuachia huru mshtakiwa huyo ambaye alikamatwa tena mahakamani hapo hapo na kisha kuunganishwa na wenzake hao na kusomewa kesi mpya.
Washitakiwa, Bulenganija, Kisena na Lubuye wamesomewa mashtaka yao leo Septemba 18, 2023 na wakili wa serikali Fatuma Waziri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.
Inadaiwa, Octoba Mosi, 2011 washtakiwa walighushi mkataba wa uongo wa kukodisha eneo kati ya UDA na Kampuni ya Simon Group Limited, kwa gharama ya sh milioni 400 kwa mwaka ndani ya miaka 10, katika eneo lililipo Kurasini lenye ekeri 13, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Washtakiwa pia wanadaiwa kujipatia Sh. bilioni 14 kutoka UDA wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la kwanza la kughushi.
Katika shitaka la tatu inadaiwa kati ya Mei Mosi, 2011 na Desemba 12, 2022 , kwa nia ovu washtakiwa waliiba fedha sh bilioni 14 na kusababisha shirika hilo kupata hasara.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ama kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Octoba 2, 2023 kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa makosa yanayowakabili hayana dhamana.
Post a Comment