MASOMO YA IMANI KUPUNGUZA MMOMONYOKO WA MAADILI.
Na Nasra Ismail ,Geita
Jamii imeaswa kuwafundisha watoto katika misingi ya imani ya dini ili wakue katika hofu ya Mungu na makatazo yake ili kupunguza wimbi kubwa na mmomonyoko wa maadili na vitendo ya kikatili kwa watoto.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa taasisi za Royal Family schools Eng Lazaro Philipo zinazopatikana mkoani Geita wakati wa mahafali ya kuwaaga darasa la saba.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mahafali hayo Lazaro alisema kuwa katika shule hizo watoto wanafundishwa maswala ya kiimani zaidi hivyo inawasaidia kuzalisha watoto wenye hofu ya Mungu.
Aidha alitoa wito kwa wamiliki wa shule zingine kuendeleza utaratibu huo wa kuwajenga watoto katika imani ili huko mbeleni kuwe na kizazi chenye maadili.
"Tunapokuja kwenye eneo la maadili, maadili ndio kila kitu, huwezi kuwa na elimu bora halafu maadili mabovu haitasaidia kwa hapa kwetu huu ndio msingi wetu maadili bora" Alisema Lazaro
Nae mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Nyang'wale Grace Kingalame aliongeza kuwa suala la maadili ni la wote hivyo wazazi washiriki katika kuwajenga watoto hawa katika maadili na sio kuwatelekezea walimu tu.
"Lakini pia mimi kama mzazi niliona ni vema tukumbushane kwamba swala la maadili ni swala mtambuka linanihitaji mimi na wewe" Alisema Kingarame.
Aidha bi kingarame aliongeza pia kuwa suala la masomo ya vitendo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi kubwa ya vijana ambao hawana ajira kwani wataweza kujiajiri wenyewe.
"Kama mtu amejifunza maswala ya uselemala akianzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza vitanda, makochi maana yake huyo anatengeneza ajira kwa wengine pia" alisema Kingarame.
Nao wazazi waliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuhakikisha watoto wanasoma masomo ya dini na kuyaelewa hivyo kuwa na hofu ya madhambi na kupunguza mmomonyoko wa maadili.
Post a Comment