Header Ads

test

RC GEITA AIPONGEZA GGML KUDHAMINI MAONESHO YA MADINI, 400 KUSHIRIKI

Na Mwandishi Wetu, Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita ambayo mwaka huu yanashirikisha zaidi ya washiriki 400.

Hatua hiyo imekuja baada ya maonesho hayo kuzidi kuwa na mvuto wa kipekee na kushirikisha washiriki kutoka nje ya nchi ikiwamo Burundi, China, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 21 Septemba 2023 kuhusu maandalizi ya maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili mjini Geita, Mkuu huyo wa mkoa amesema mwaka jana walishiriki walikuwa zaidi ya 250.

Amesema mkoa wa Geita umeweka mazingira mazuri kwa kampuni zinazojihusisha na utafiti wa madini, uchimbaji unaotumia teknoljia rahisi, uchenjua pamoja na uongezaji thamani ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kukua kibiashara.

“Niwakaribishe wawekezaji kuwekeza viwanda vya uchenjuaji pamoja na uongezaji thamani ili kuwaelimisha wananchi na wachimba wetu kuondokana na matumizi ya kemikali hatari kama vile zebaki. Pia niwakaribishe wananchi wote hasa wanaojihusisha na uongezaji thamani. Niwaombe waje kwa wingi kwa sababu maonesho yameanza jana tarehe 20 Septemba 2023,” amesema.

Amesema maonesho hayo yatafunguliwa rasmi tarehe 23 Septemba 2023 na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati. Maonesho hayo yatafungwa na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 30 Septemba 2023.

Aidha, akizungumzia ushiriki wa GGML katika maonesho hayo mjini Geita jana, Meneja Mwandamizi wa kampuni hiyo anayesimamia mahusiano jamii, Gilbert Mworia alisema maonesho hayo yamekuwa na mvuto wa kipekee tangu yalipoasisiwa kutokana na ufadhili wa GGML kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambao uliwezesha ujenzi wa eneo hilo la EPZA pamoja na eneo la uwanja huo wa maonesho.

Amesema GGML imekuwa kinara wa kuboresha maonesho hayo kwa kuwekeza Sh 800 milioni katika ujenzi wa jengo la utawala la EPZA.

"Msaada wetu unavuka usaidizi wa kifedha ambao tumeendelea kuutoa kila mwaka, kwa sababu tulitoa msaada wa maandalizi ya maonesho hayo kama vile mahema, jenereta la dharura na mafuta yanakayotumika kwa wakati wote wa maonesho,” alisema Mworia.

Aidha, amesema ili kutimiza malengo ya muda mrefu ya ukuaji wa uchumi endelevu, GGML inaunga mkono Dira ya 2025 ya serikali. Mpango huu unalenga kuiwezesha sekta ya uchimbaji madini kukua na kufikia kiwango cha asilimia 10 kwenye Pato la Taifa la Tanzania.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella (kushoto) akiteta jambo na Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulia mahusiani ya jamii, Gilbert Mworia (katikati) katika viwanja vya Bombambili Geita kunakofanyika maonesho ya teknolojia ya madini Geita. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella (kushoto) akiteta jambo na Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulia mahusiani ya jamii, Gilbert Mworia (katikati) katika viwanja vya Bombambili Geita kunakofanyika maonesho ya teknolojia ya madini Geita. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Zahara Michuzi.

No comments