RC MONGELA AWATAKA WASTAAFU MFUKO WA PSSSF KUACHA MIHEMKO KUANZISHA MIRADI MIKUBWA ITAKAYOWAPA MAWAZO
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela akitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya maandalizi ya wastaafu kwa wastaafu watarajiwa wa mfuko wa PSSSF
Kaimu Mkurugenzi wa mfuko wa pensheni wa PSSSF Mbaruku Magawa akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela zawadi wa mti ikiwa ni moja ya kampeni za mfuko huo kupanda miti milioni Moja (1000,000) kufikia Disemba mwaka huu 2023
washiriki wa semina wastaafu watarajiwa wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akipatia mmoja wa wastaafu watarajiwa zawadi ya mti
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Mbaruku Magawa akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela.
Wastaafu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela(hayupo pichani) ambaye amewataka kujitayarisha mapema kabla ya kustaafu
Na Seif Mangwangi, Arusha
SERIKALI imewataka wastaafu wanaotarajia kustaafu utumishi wao kuanza kufanya maandalizi ya kustaafu kwao mapema ikiwemo kubuni miradi ambayo wataweza kuifanya baada ya kutoka kazini ili kuwa rahisi kuiendeleza.
Aidha watumishi hao wametakiwa kutumia sehemu ya fedha za mafao watakazolipwa baada ya kustaafu kuziwekeza kwenye miradi itakayowaletea tija na ambayo itaweza kudumu kwa kipindi kirefu na kuepuka kuanzisha miradi kwa mihemko.
Wito huo umetolewa leo Septemba 19, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alipokuwa akifungua semina ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa wa mfuko wa hifadhi ya Jamii PSSSF wa Mkoa wa Arusha.
Mongela amesema wastaafu wengi wamekuwa wakipoteza maisha mara tu baada ya kuhitimisha utumishi wao kazini kutokana na kukutwa na msongo wa mawazo yanayosababishwa na kutojipanga mapema kabla ya kustaafu.
“Kustaafu utumishi wa umma ni jambo la lazima sio hiyari lakini lazima ujiulize kabla ya kustaafu umejipanga kuishi maisha gani baada ya kustaafu?, hili swali ni muhimu sana kujiuliza ili uweze kuishi maisha marefu zaidi mpaka Mungu atakapokuita,”amesema.
Amesema Serikali inawapenda wastaafu na ingependa kuendelea kuwatumia mara baada ya kustaafu utumishi wao hususani kwenye shughuli za kijamii ambazo zinahitaji watumishi wenye maarifa mengi ambayo wastaafu tayari wanayo.
“Afya zenu ni muhimu sana, kwetu sisi kama Serikali, tunawapenda na tungependa kuendelea kufanyakazi na nyie, mkistaafu mtakuwa kijijini ambapo kuna nafasi nyingi za siasa ambazo pia zinahitaji watu wenye maarifa na uzoefu, tungependa kuona mnaendelea kuwa na afya nzuri ili muweze kuisaidia Jamii kwenye nafasi kama hizi,”amesema na kuongeza:
“Ningewashauri mkistaafu msiende kuanzisha miradi kwa mihemko, miradi mingine ni kukukimbizia kaburini, mfano umepokea mafao yako unaenda kununua daladala, huu ni mradi ambao unahitaji kuendeshwa na wazoefu, anzisheni miradi ambayo mtaweza kuifuatilia na hata kuiendesha wenyewe,”amesema.
Amesema katika semina hiyo taasisi mbalimbali zimeweza kutoa elimu ya uwekezaji wa fedha ikiwemo taasisi za kibenki, hivyo ni wakati wao kutafakari kwa makini ni wapi wawekeze kwa faida kubwa.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa PSSSF, Mbaruku Magawa amesema mfuko wa PSSSF umeamua kutoa elimu ya uwekezaji kwa wastaafu watarajiwa wa mfuko huo ili kuwajenga kisaikolojia na kuwaondoa kwenye msongo wa mawazo baada ya kustaafu.
Amesema mfuko huo umeamua kuendesha semina hiyo baada ya kuwepo kwa matukio mbalimbali ya wastaafu kupoteza maisha mapema mara baada ya kuhitimisha utumishi wao kutokana na kukosa elimu ya uwekezaji.
Aidha Magawa amesema mfuko huo unaendesha kampeni ya kupanda miti kote nchini ambapo hadi kufikia Disemba mwaka huu wanatarajia kupanda miti Milioni 1 hadi kufikia Disemba 2027 miti Milioni 7 itakuwa imeshapandwa
Post a Comment