TAFITI VETA KANDA YA KATI ZALETA TIJA KWA WAJASIRIAMALI NCHINI
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na utoaji wa huduma ya chakula na vinywaji Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma yaliyoandaliwa na VETA.
........................................................
Na Dotto Mwaibale, Bahi.
TAFITI zinazofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
Kanda ya Kati zimeanza kuonesha tija kwa wajasiriamali hapa nchini kwa
kuboresha huduma zao na kujikwamua kiuchumi.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza mwishoni mwa wiki
wakati wa mafunzo kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na upikaji
wa vyakula Mama na Baba Lishe wa Bahi mkoani Dodoma alisema mafunzo wanayoyatoa
yameanza kuonesha tija kwa walengwa hasa baada ya kupata mwanga.
"Sisi VETA Kanda ya Kati tumekuwa tukifanya utafiti katika maeneo
mbalimbali zinapofanyika shughuli za kijasiriamali ili kuona kama zinatija
ambapo tunaona sinasifa za kuweza kuwaongezea kipato kikubwa lakini inashindika
kutokana na wahusika kushindwa kujipambanua na kuendelea kufanya ujasiriamali
usiowaingizia kipato kinono licha ya maeneo yao ya kazi kuwa na wateja
lukuki," alisema Mwanja.
Alisema mpaka hivi sasa wamekwishafanya tafiti tatu ambapo kwa awamu ya
kwanza walianza mwaka jana wilayani Ikungi mkoani Singida na baada ya utafiti
wao walibaini kumekuwa na kuku wengi wa asili ambao wanahitajika kwa kiwango kikubwa
katika mikoa mbalimbali ukiwemo wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nchi lakini
wananchi wanashindwa kufuga kwa wingi nakuendelea na ufugaji ule wa kizamani
usiokwenda na soko kubwa la uhakika.
Mwanja alisema utafiti wa awamu ya pili waliufanya tena katika wilaya hiyo hiyo
baada ya kuzindua Chuo cha VETA na kubaini kuwa kumekuwa na soko kubwa la mbuzi
na kondoo wakati wa Sikukuu ya Eid Al Adha ya kuchinja ambao wanyama hao
wamekuwa wakinunuliwa kutoka mikoa mingine kutokana na Singida kutokuwanao wa kutosha.
Kwa awamu ya tatu Mwanja alisema walifanya utafiti Wilaya ya Bahi na
kugundua ni wilaya ambayo inamwingiliano mkubwa wa watu, wageni na wasafiri
wanaotumia barabara kutoka nchi za jirani kupitia mikoa ya kanda ya ziwa kwenda
Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam ambao wamekuwa wakipata chakula katika wilaya
hiyo.
“Hapa Bahi sio kwamba hakuna wajasiriamali wanao uza vyakula na vinywaji
wapo lakini bado hawafanyi vizuri katika soko licha ya kuwa katika eneo lenye
wateja wengi,madereva wa malori wanaegesha magari yao hapa kwa ajili ya
kupumzika na kupata mahitaji ya chakula na vinywaji achilia mbali mabasi,
magari madogo na watu wengine lakini wanafanya chini ya kiwango na kupata
kipato kidogo ndio maana kufuatia utafiti wetu tukaona tuwaite na kuwapa
mafunzo hayo yatakayowasaidia kubadilika na kukiingia katika ujasiriamali wa
viwango na wenye tija.
Alisema mafunzo hayo yanagharamiwa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan na VETA kazi yao ni kufanya utafiti na kuwatoa wataalamu ambao
uwafundisha wajasiriamali hao kulingana na mahitaji ya eneo husika.
“Kipee nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa
kuliona jambo ili jema analolifanya kwa wananchi wake kwa kutoa fedha nyingi
ambazo zinakwenda kubadilisha maisha yao kwani wengi wao wanauwezo mkubwa wa
kujitafutia riziki lakini hawana uelewa mpana wa kufanya shughuli zao ili
wasonge mbele kimaisha na ndio maana tunakutana nao na kuwapata mafunzo haya bure,”
alisema Mwanja.
Alisema VETA Kanda ya Kati ambao wanahudumia mikoa ya Singida, Manyara na
Dodoma wamejipanga kuendelea kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwa ni
kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia za kuhakikisha wananchi wanabadilika
kiuchumi kwa kujitegemea kutokana na fedha anazozitoa kwa ajili yao.
Mwanja alitumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wananchi wa wilaya ya Bahi
kuwahimiza watoto wao ambao wamemaliza masomo yao ya shule ya msingi, sekondari
na vyuo vikuu lakini wapo nyumbani kwa sababu moja au nyingine kwenda kujiunga
na Chuo cha VETA kilichojengwa wilayani humo kupata stadi za ufundi ambao
unaweza kuwasaidia kujiajiri badala ya kuajiriwa na kuondokana na changamoto ya
soko la ajira ambao baadhi yao wakekuwa wakipata msongo wa mawazo na kufikia
hatua ya kujiua kwa kukosa kazi.
Alisema chuo hicho ujenzi wake umekwisha kamilika kwa asilimia 100 na kuwa
kitaanza kuendesha mafunzo ya kozi ndefu na fupi na kuwa ya muda mrefu yatachukua
muda wa miaka miwili hadi mitatu ambayo yatatolewa katika fani zipatazo sita
katika awamu ya kwanza ambazo ni Uhazili na Kompyuta (Secretarial and Computer
Application),Ushonaji (Design Sewing and Cloth Technology), Uashi (Masonry and
Bricklaying),Umeme wa Majumbani (Electrical Installation),Ufundi Magari (Motor
Vehicle Mechanics) na Uchomeleaji Vyuma (Welding and Metal Fabrication).
Alisema chuo kitaanza kudahili wanafunzi januari mwakani na kuwa nafasi
zipo za kutosha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Zaina Mlawa akizungumza wakati akifungua
mafunzo hayo aliwataka washiriki kuzingatia yale ambayo watafundishwa kwani ni
mafunzo yenye tija na yana kwenda kuinua maisha ya familia za wana Bahi na
taifa kwa ujumla.
"Mahitaji ya chakula katika hili eneo letu la Bahi ni makubwa mno
kutokana na kuwa na wageni wengi na muingiliano wa watu mbalimbali zingatieni
mafunzo haya yatawaongezea kipato na kuweza kujikimu kimaisha na familia zenu
kutokana na huduma nzuri mtakazo zipata na halmashauri yetu itapata mapato
kutokana na kodi mtakayokuwa mkilipa,” alisema Mlawa.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mwalimu wa Fani ya Upishi VETA Kanda ya Kati
Dodoma, Adelina Edward, alisema mafunzo hayo kwa wapishi na watoa huduma ya
chakula ni ya muhimu sana na kuwa wameyafanya kufuatia utafiti walioufanya
katika wilaya hiyo.
Alisema katika utafiti huo waligundua kuwa watoa huduma wa chakula wa
wilaya hiyo katika maeneo kadhaa ya ufanyaji kazi zao wamekuwa na changamoto za
hapa na pale zikiwemo za namna ya kutunza kumbukumbu, usafi wa chakula,lugha
nzuri kwa wateja, uvaaji wenye staha na mambo mengine mengi ambayo yanafanana
na hayo ambayo wanapaswa kuyafanya.
Alitaja baadhi ya maeneo waliyoyafundisha kwenye mafunzo waliyotoa kuwa ni
huduma bora kwa wateja na mbinu zitakazotumika ili mteja aridhike na huduma
zao, kumjua mteja anayemuhudumia na eneo ambalo huduma zao zilipo.
Edward alisema eneo lingine walilowafundisha ni namna ya kumjua mteja kama
atakuwa ameridhika baada ya kuhudumiwa chakula na aina ya mteja anayehudumiwa.
“Ni muhimu kwa mtoa huduma wa chakula na vinywaji akaifahamu vizuri bidhaa au huduma anayoitoa kwa mteja wake kwani wapo baadhi ya wateja wanahitaji maelezo ya kina ili aweze kushawishika na huduma yako,” alisema Edward.
Washiriki wamafunzo hayo Semeni Athumani, Nicholaus
Machimo, Charles Aman na Christina Wilson waliishukuru sana VETA kwa
kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewaongezea uelewa mkubwa wa utunzaji wa
kumbukumbu za mauzo yao jambo ambalo walikuwa hawalifanyi.
“Tulikuwa tunafanya ujasiriamali wetu bila ya kutunza kumbukumbu lakini
sasa tunakwenda kununua madaftari matatu kama tulivyoelekezwa kwa ajili ya ya
utunzaji wa kumbukumbu zetu ambayo ni la mauzo, manunuzi na gharama nyinezo
kama matumizi ya umeme, kodi, usafiri na mengineyo na kuwa biashara bila ya
daftari hupotea bila ya habari,” alisema Wilson.
Semeni Athumani alisema anaishukuru VETA kwa kuwapelekea mafunzo hayo kwani
sasa wamejua namna ya kuwahumia wateja wa muda mfupi kama wanaofanya kazi za
ukandarasi ambao wanatakiwa kulipa papo kwa papo baada ya kuhudumiwa kwani
walikuwa wakiwakopesha na mradi ukiisha wanaondoka bila ya kuwalipa jambo
ambalo lilikuwa likiwapa changamono ya kuwatafuta viongozi ambao mradi husika
upo ili wawasaidie kupata fedha zao bila ya mafanikio.
Washiriki hao kwa pamoja walitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kuwakumbuka watu wenye vipato vya chini kwa kutoa fedha hizo kwa
ajili ya mafunzo hayo walipewa kupitia wataalam kutoka VETA.
Aidha walimshuru Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja na watumishi wenzake tendaji wake kwa jinsi walivyojitoa kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yanakwenda kubadilisha maisha yao kupitia fursa za utoaji wa huduma kwa wateja wao na wakaomba mafunzo hayo yawe endelevu kwani kuna wenzao wengi ambao hawajabahatika kuyapata.
Post a Comment