Header Ads

test

MRADI WA 2D UTAFUTAJI MAFUTA EYASI WEMBERE WAKAMILIKA

Na Janeth Mesomapya na Regina Masolwa

MRADI Wa kuchukua data za mitetemo za 2D katika kitalu cha Eyasi Wembere umefikia mwisho huku wataalamu wakieleza kuwa na matumaini ya utafiti huo kubainisha na kuainisha maeneo yenye viashiria vya uwepo wa rasimali ya mafuta.

Hayo yamebainika hivi karibuni wakati wa ziara ya ufuatiliaji iliyofanywa na Maafisa wa Mamlaka ya udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) katika eneo la Eyasi Wembere mkoani Singida ambapo mradi huo umekuwa ukitekelezwa.

Akizungumza na maafisa hao Bw. Sindi Maduhu, Mjiofizikia wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Meneja Mradi huo ameeleza kuwa utafiti huo wa 2D umefanyika katika maeneo yaliyopo katika wilaya sita zilizo ndani ya mikoa mitano ambayo ni Singida, Arusha, Tabora, Shinyanga na Simiyu.

“Tuna matumaini makubwa kuwa utafiti huu utatusaidia kubainisha na kuainisha maeneo yenye viashiria vya uwepo wa mafuta na gesi asilia na endapo tutagundua viashiria na kujiridhisha na uwepo wa rasilimali hiyo, hapo ndipo itaanza hatua muhimu ya kuchoronga visima vya utafiti zaidi,” alisema.

Akieleza historia fupi ya utafiti wa mafuta kwenye bonde hilo la Eyasi Wembere Bw. Maduhu ameeleza kuwa utafiti ulianza mwaka 2015 kwa kuchukua taarifa za kijiofizia (gravity magnetic) ili kubaini ukubwa wa eneo la bonde na kuangalia kina cha miamba tabaka iliyopo katika eneo husika.

Eneo la Eyasi Wembere lina kilometa za mraba 10630, na utafiti huo ulilenga kusoma aina na kina cha miamba ili kubaini uwezekano wa uwepo wa mafuta au gesi asilia katika eneo husika.

Utafiti katika bonde hilo umekuwa ukiendelea kufanyika kwa vipindi tofauti tofauti na kwa kutumia teknolojia mbalimbali ambapo kufikia mwezi Julai 2023 utafiti wa data za mitetemo kwa njia ya 2D ulianza rasmi kwenye eneo hilo.

Bw. Maduhu alifafanua kuwa utafiti wa data za mitetemo (2D) ni ule wa kutuma mawimbi ya sauti ardhini na mawimbi hayo hurudisha taarifa ambazo baadaye huchakatwa na kutafsiriwa ili kuielewa miamba ya eneo husika na hivyo ili kujiridhisha na viashiria vya uwepo wa mafuta.

Akizungumzia ushiriki wa wazawa kwenye mradi huo, Bw. Maduhu amesema Watanzania wengi wamenufaika na nafasi za ajira katika kipindi chote cha utekelezaji mathalani mwaka 2022 zaidi ya Watanzania 40 waliajiriwa kwa ajira za muda ili kufanya kazi ya kukusanya taarifa za kijiokemia.

Aidha alibainisha kuwa tangu kuanza utafiti wa 2D mwezi Julai, zaidi ya Watanzania 250 wamepata ajira katika mradi huo huku takriban asilimia 98 ya kazi za kitaalamu zikifanywa na wazawa ikiwa ni pamoja na kazi za kuendesha mitambo huku ikilinganishwa na asilimia 2 pekee iliyohusisha raia wa kigeni.

“Kwa upande wa manunuzi zaidi ya asilimia 60 ya kandarasi zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huo ni za kampuni za Kitanzania ikiwa ni pamoja na kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS) ambayo ndiye mkandarasi aliyefanya utafiti husika wa 2D kwenye mradi huu,” alieleza.

Aliongeza kuwa kandarasi ndogondogo za kutoa huduma kama chakula, ulinzi na nyinginezo ndizo zilizopewa kipaumbele kwenye mradi huo ikilinganishwa na kampuni za kigeni.

Mradi huu wa kuchukua data za mitetemo katika bonde hilo la Eyasi Wembere umegharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 8 ambazo zimetolewa na Serikali kupitia TPDC.
Wataalamu wakiwa kwenye shughuli ya kuchoronga mashimo ya kuchukua data za mitetemo za 2D katika mradi utafutaji wa mafuta katika Kitalu cha Eyasi Wembere.

No comments