SATF YAJIVUNIA MAFANIKIO LUKUKI TANGU KUANZISHWA KWAKE MIAKA 25 ILIYOPITA, YAFIKIA WATOTO 210, 000
Mwenyekiti wa Bodi ya SATF Bi. Mariam Mwaffisi (kushoto) akishiriki katika utoaji vyeti kwa wadau mbalimbali. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa SATF, Bi Beatrice Mgaya na Meneja wa Miradi, Nelson Rutabanzibwa.
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Social Action Trust Fund (SATF) katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kusaidia zaidi ya watoto 210,000 nchini kuwatoa katika mazingira hatarishi, kuwawezesha kujitegemea na kuchangia katika pato la taifa.
Shirika hilo lilianzishwa kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Serikali ya Marekani April,1998 na kuratibiwa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika mjadala maalumu wa wadau wa taasisi hiyo kwaajili ya maadhimisho ya miaka 25, uliofanyika jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake wa mwaka, Mkurugenzi wa SATF Beatrice Mgaya, amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya taaisisi yake na wadau mbalimbali katika ngazi husika.
Amesema taasisi ya SATF imekuwa ikifadhili elimu ya msingi, sekondari, ufundi na vyuo vikuu, huduma za afya, lishe, ulinzi wa mama na mtoto kwa kuzijengea uwezo kamati za kuratibu shughuli za ulinzi wa mama na mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili (MTAKUWA) uimarishaji wa uchumi na kaya zenye watoto walio katika mazingira hatarishi, kutoa msaada kwa Watoto wenye mahitaji maalumu na kugawa madawati, magodoro na vitanda kwa shule za serikali zenye uhitaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi, msaada na ufadhili wa SATF umekuwa ukipitia katika asasi na taasisi zisizo za kiserikali zinazoaminika ambazo zinatekeleza miradi ya SATF katika Halmashauri 36 za Tanzania Bara kwa sasa.
“Hii ni rekodi nzuri na ya kujivunjia na ninaamini kwamba SATF inatendelea kuisadia jamii kwa kuhakikisha watoto wetu ambao hawana uwezo wanafikia ndoto zao.
"Hadi sasa tuna wanafunzi ambao tuliwafadhili tangu ngazi ya msingi hadi chuo kikuu na wengine wameajiriwa, kwetu sisi hilo ni jambo la kujivunia,” amesema Mkurugenzi wa SATF.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya SATF Mariam Mwaffisi ameelezea kufurahishwa na hatua hiyo ya mafanikio huku akiushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa utendaji uliotukuka.
“Mafanikio kama haya hayaji hivi hivi bali ni kutokana na uongozi bora na wakichapa kazi tulionao hapa SATF. Niwapongeze kwa hatua hiyo. Kama kuna mtu anataka kujifunza namna ya kuongoza taasisi kuwa endelevu, aje SATF achukue mfano wake,”amesema Mwaffisi.
Katika maadhimisho hayo ya miaka 25, taasisi hiyo imetumia fursa hiyo kukutana na wadau wake kwa lengo la kutafakari mafanikio na changamoto ndani ya miaka 25 ya kuhudumia jamii ya Tanzania, pia kuzijengea uwezo asasi zinazototekeleza miradi ya SATF kuhakikisha afua zinazotekelezwa zinajikita katika malengo endelevu ya dunia kwa kuzingatia mipango na miongozo ya kitaifa.
“Si hivyo tu bali tumeamua wakati wa maadhimisho iwe fursa pia ya kuendelea kuwajengea uwezo wadau wetu ili wapate ujuzi zaidi wa kuendelea kutekeleza miradi ya SATF kwa ufanisi bora zaidi,” amesema Meneja wa Miradi ya SATF, Nelson Rutabanzibwa.
Post a Comment