T-PESA YATOA ELIMU KWA WATEJA KWENYE MAADHIMISHO WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA
KAMPUNI Tanzu ya
Shirika la Mawasiliano Tanzania, T-PESA imesema kuwa uwepo wa Maadhimisho ya
Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa umeleta chachu katika utoaji wa elimu kwa
Wateja wake na Wananchi kwa ujumla kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na
Kampuni hiyo.
Hayo yameelezwa na
Afisa Uhusiano wa TTCL, Bi. Adeline Berchimance akizungumza katika Maadhimisho
ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika Viwanja vya Shekhe Amri Abeid jijini
Arusha.
Amesema Maadhimisho
hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na kuzishirikisha Taasisi ndogo za
fedha, Mabenki, Mifuko ya Hifadhi za Jamii pamoja na wajasiriamali yameisaidia
Kampuni ya T-PESA kukutana na Wananchi na kuwajengea uelewa kuhusu matumizi
sahihi ya fedha mtandao na fursa mbalimbali zinazopatikana katika Kampuni hiyo
zinazoweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Amesema katika kuunga
juhudi za Serikali za kutatua changamoto ya ajira kwa vijana T-PESA imetoa fursa
mbalimbali kwa vijana zinazoweza kuwasaidia kujitengenezea kipato na hivyo
kujikwamua kiuchumi.
"T-PESA inazo
fursa mbalimbali hasa kwa vijana ikiwa ni pamoja na uwakala ambapo wanaweza
kufanya biashara hii ya kuwa Wakala na kujipatia kipato cha kusaidia familia
zao kwani T-PESA tunatoa kamisheni kubwa zaidi ukilinganisha na mitandao
mingine," amesema Bi. Adeline.
Aidha amesema
Maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine yametoa fursa kwa Kampuni hiyo
kukutana na Wateja na Wananchi kwa ukubwa zaidi na kujibu hoja, maswali na kero
zao na hivyo maadhimisho hayo yamekuwa muhimu katika kupata mrejesho sahihi
kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na T-PESA.
Maadhimisho ya Wiki ya
Huduma za Fedha Kitaifa yanafanyika kwa mara ya tatu sasa huku kwa mwaka huu
yakibeba kaulimbiu ya, ‘Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Uchumi na
kuzinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa (Mb) na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali.
Bw. Peter Mushi, Afisa Mauzo Shirika la Mawasiliano Tanzania akitoa elimu kuhusu huduma za T-PESA kwa kwa wakazi wa Arusha walipotembelea Banda la T-PESA wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu 'Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Uchumi yanayoendelea katika Viwanja vya Shekhe Amri Abeid jijini Arusha. |
Post a Comment