WATAALAMU, VIFAA VYA KISASA, VYAWEZESHA HUDUMA BORA KWA WATOTO WANAOZALIWA KABLA YA WAKATI MLOGANZILA
Uwepo wa wataalamu na vifaa tiba vya kisasa vya kuhudumia mama na mtoto vimewezesha kusaidia kuboresha huduma za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Hayo yamesemwa leo kwa niaba ya Naibu Mkurugeni Mtendaji na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba MNH-MLOGANZILA Dkt. Faraja Chiwanga wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto anayezaliwa kabla ya wakati.
"Kwa sasa hakuna sababu kwa mtoto anayezaliwa kabla ya wakati kupata shida, sababu tuna wataalamu wenye uwezo na vitendea kazi vya kisasa" amesema Dkt. Chiwanga
Amesema Mloganzila kuna wodi ya kuhudumia watoto wachanga mahututi wenye umri kati ya siku 1 hadi 28 iliyosheheni vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine za kisasa za kusaidia watoto kupumua pamoja na kutibu homa ya manjano, uhakika wa upatikanaji wa dawa.
Kwa Upande wake Daktari Bingwa wa Watoto na Mkuu wa Idara ya Watoto MNH-MLOGANZILA Dkt. Mwanaidi Amir, amesema kuwa idara hiyo imeadhimisha siku hii kwa kufanya matembezi ya hisani ili kueneza uelewa kuhusu masuala ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, kutoa elimu ya matunzo ya watoto hao, pamoja na kuwafanyia vipimo vya msingi watoto ambao walizaliwa kabla ya wakati ili kubaini kama wana changamoto yoyote katika makuzi yao.
Siku ya kimataifa ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati huadhimishwa Novemba 17 kila mwaka ambapo mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo "Hatua kidogo, Faida kubwa: Huduma ya ngozi kwa ngozi , kwa kila mtoto,kila mahali"
Post a Comment