SHAMBA LA MBEGU NAMTUMBO KUWA SEHEMU YA UTALII WA KILIMO NCHINI
Na Albano Midelo,Namtumbo
WILAYA ya Namtumbo mkoani Ruvuma msimu huu imepata Mwekezaji wa kulima na kuzalisha mbegu bora za mahindi katika shamba lenye ukubwa wa hekta 1,600.
Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Ngollo Malenya amesema serikali pia imelima shamba la mbegu za mahindi na alizeti katika shamba lenye ukubwa wa hekta 2,000.
“Serikali inatarajia kujenga ukuta kwa ajili ya kuboresha ulinzi na mfumo wa umwagiliaji,pia serikali imepanga shamba hilo kuwa sehemu ya utalii wa kilimo hapa nchini’’,alisisitiza DC Malenya.
Ameongeza kuwa katika eneo hilo kutakuwa na shule ya kilimo na kwamba zitajengwa hosteli za kisasa kwa ajili ya wageni na watalii watakaofika kufanya utalii wa kilimo katika shamba hilo.
Amesema shamba hilo la aina yake nchini,litaongeza wigo wa ajira kwa wazawa hali ambayo pia itaongeza mapato na kuinua uchumi kwa wananchi na Wakala wa Mbegu nchini.
Katika msimu uliopita Wilaya ya Namtumbo ilizalisha mazao tani 12,500 na msimu huu wilaya inatarajia kuzalisha mazao zaidi ya tani 25,000.
Post a Comment