Header Ads

test

Alliance One yatoa msaada wa 25m/- kwa waathirika janga la Hanang’

Na Mwandishi Wetu, Hanang'

Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One yenye makao yake makuu mkoani Morogoro jana imekabidhi msaada wa bidhaa mbalimbali kwa waathirka wa janga la maporomoko ya ardhi huko Katesh,Wilayani Hanang, bidhaa hizo zikiwa na thamani ya milioni 25. 

Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti amesema kampuni imepokea kwa majonzi taarifa za majonzi ya mkasa wa Hanang, na hivyo inampa pole sana Mheshimiwa Rais wa jamhuri ya Samia Suluhu Hassan kwa kupoteza watanzania kwa janga hili lililotokea huko na kusababisha makumi ya vifo vya watu.
 
“Kampuni ya Alliance one kama kupitia sera yake ya uwajibikaji kwa jamii, Mkurugenzi Mkuu pamoja na managementi yote tumefikiria na kufikia uamuzi kuwa tutoe misaada mbalimbali ikiwemo lishe ya watoto wadogo yaani baby formula, mavazi kwa ajili ya familia nzima zote kwa maana ya watu wazima na wadogo nguzo ambazo ni mpya,”alisema.

Aliongeza kuwa vilevile katika kuwasitiri waathirika hao ambao wamepoteza vitu vyao,wamepeleka mablanketi, ambayo yatatumika kuwasitiri kwa namna moja au nyingine.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw.Francis Namaungo alisema alitoa shukrani tele kwa kampuni hiyo ambapo alisema wananchi wa Hanang wanaipokea misaada hiyo kwa moyo mkunjufu. 

“Misaada huu kwa waathirika hawa wa maporomoko ya matope, magogo, mawe na takataka zingine kwa walengwa hawa umekuja kwa wakati muafaka,” alisema.

Akitolea mfano alisema hii lishe mlioleta kwa ajili ya watoto, ambao ni taifa la kesho, kwa kupatiwa lishe bora, watoto wadogo hawa watakuja kumudu vyema majukumu yao kwa taifa lao ukubwani.

“Lakini pia kwa mavazi, zikiwemo jeans na tishiti, zitawasaidia sana, kwani wengi wao waliondokewa kabisa na mavazi,chakula, mali zao wakati wa janga hili,kwa hiyo hili linagusa msaada mkubwa katika maisha yao,” alisema.

Kwa niaba ya wanahanag wote nasema asante, ninachowahakikishia tu ni kwamba msaada huu utawafikia walengwa wanaostahili kadri, ambavyo utaratibu wa kiserikali kwa idadi ya waliopata maafa na idadi ya misaada uliotolewa watapewa kwa uwiano unaotakiwa.

Karibuni tena waambieni na wengine kwamba tunahitaji na vifaa vya ujenzi,kwa sababu wapo pia waliopoteza makazi, kwa hivyo tunafanya utaratibu wa kuangalia kuwarejesha katika makazi pengine kwa kuwajengea, hivyo mahitaji ya ujenzi huo yanahitajika pia.

Naye mmoja wa waathirika wa mkasa huo ambao wamehifadhiwa kwenye shule ya sekondari ya Katesh, Bi.Zepetu Murda alisema hakutoka na kitu chochote mkononi siku ya janga hilo zaidi ya uhai wake tu. 

“Kwa mfano mimi nilitoka kwenye nyumba yangu nikiwa uchi wa mnyama,Wasamalia wema walipokuwa wananiokoa ndio walinifunika kwa mavazi yao na kunisitiri nguo hizi na zingine ninazoendelea kupewa na wasamalia wema,” alisema na kuongeza kuwa anategemea sana msaada wa serikali na wasamalia wema ndio utakaowasaidia kutoka katika hali waliyonayo.

Mwathirika mwingine Stephano Robert ambaye naye miongoni mwa kundi la mwisho la waathirika walosalia shuleni hapo,alisema tukio hilo lilitokea kwa namna ya kushutukiza saa 12:15 asubuhi na lilikuwa ni tope.

Alisema walichofanya ni kutafuta namna ya haraka kujiokoa kwa kukimbilia kwa majirani kwani nyumba zao tayari zilikuwa zinazidi kujaa tope huku likiongezeka.Wakati wa mbio hizo vyombo vyao walivitelekeza na hawana kitu walichosalia.

Wapo wengi waliopoteza maisha,wengine ni majirani zao lakini wao walinusurika na wanamshukuru Mungu kwa uzima walionao na wanaamini watasaidika na misaada inayoendelea kuletwa.

Kampuni ya Alliance One katika mpango wake wa huduma kwa jamii inatenga 400m/- kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii katika maeneo ya maji, elimu na afya.

Alliance One ilifungua kiwanda chake cha usindikaji mnamo 1998 na imekuwa inafanya kazi kwa mafanikio tangu wakati huo bila kukosa msimu wowote wa mazao na kwa sasa ina wafanyikazi 350 wa kudumu na wanaolipwa pensheni pamoja na wafanyakazi wa msimu 3,000 kila mwaka.


Msemaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One Wakili John Magoti,(kulia) akimkabidhi fulana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang',Bw.Francis Namaumbo, kama sehemu ya msaada wa bidhaa mbalimbali zenye thamani ya 25m/- kwa ajili waathirika wa janga la maporomoko ya ardhi yaliyotokea wilayani humo.Vifaa vingine vilivyotolewa ni mablanketi,unga wa lishe na suruali na sketi kwa ajili ya waathirika hao

No comments