Na Mwandishi wetu, Dodoma Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wameendesha mafunzo ya
kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa TEHAMA wa taasisi hiyo. Akizungumza wakati wa mafunzo hayo,
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Bw. Kailima Ramadhani, amesema kuwa Mafunzo
haya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi wa teknolojia ya habari na
mawasiliano katika taasisi hiyo. Amesema Tume inajitahidi kuwekeza
katika TEHAMA, hasa kwa kutumia vifaa vya BVR (Biometric Voter Registration)
katika uandikishaji wa wapiga kura, pamoja na mifumo ya kusimamia daftari,
matokeo, wagombea, na waangalizi wa uchaguzi. Aidha, Bw.Kailima amesema tayari Tume
imepitisha miongozo saba ya kisera ili kuimarisha matumizi sahihi ya TEHAMA
katika shughuli zake. Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na sheria zinazohusiana na usimamizi wa
teknolojia katika taasisi za umma. Bw. Kailima ameitaja Miongozo
iliyopitishwa kuwa ni pamoja na Sera ya TEHAMA, Mpango Mkakati wa TEHAMA,
Mpango wa Kujikinga na Majanga ya TEHAMA, Sera ya Usalama wa TEHAMA, Mwongozo
wa TEHAMA, Mwongozo wa Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, na Mwongozo wa Uundaji wa
Mifumo ya TEHAMA.
Nae Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),
Bw. Stanslaus Mwita amesema licha ya kuwa Tume ipo katika utekelezaji wa jukumu
kubwa la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini wanatambua
umuhimu wa mafunzo hayo. “Kwa
sasa Tume inajukumuku kubwa la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
lakini kwa kutambua umuhimu wa mafunzo haya na nasisi kama watumiaji wa kubwa
wa mifumo ya TEHAMAili kuhakikisha kama
taasisi inafuata sera na miongozo iliyowekwa,”
alisema Mwita. Kiongozi wa Timu ya wakufunzi ambaye
ni Meneja wa Usimamizi na Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao (e-GA) Bi.
Sultana Seif, amesema wanaendesha mafunzo kwa Kamati hiyo ya Uongozi wa TEHAMA
ya Tume ili kuhakikisha wanaelewa na kuzingatia matakwa ya sheria ya serikali
mtandao pamoja na viwango na miongozo.
Post a Comment