WATANZANIA WAHAMASISHWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UCHAGUZI MKUU WA 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 31,2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 31,2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg Kailima Ramadhani akitoa mada wakati wa Kikao cha Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 31,2025.
Washiriki wa Mkutano huo wakifuatilia mada.
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeyataka makundi mbalimbali ya kijamii nchini kuyatumia majukwaa yao kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeyataka makundi mbalimbali ya kijamii nchini kuyatumia majukwaa yao kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo, tarehe 31 Julai 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano kati ya Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu.
Katika hotuba yake, Jaji Mwambegele ameeleza kuwa Tume inatambua na kuthamini mchango wa watu wenye ulemavu katika kueneza taarifa sahihi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.
“Nawasihi kutumia majukwaa yenu kuhimiza wenzenu kushiriki kwa amani na kuepuka kauli au vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi yetu wakati wa kampeni,” amesema Mhe. Mwambegele, na kuongeza kuwa Tume itaendelea kushirikiana nao katika hatua zote muhimu kuelekea uchaguzi.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu, Jaji Mwambegele amesema kuwa ratiba rasmi imeshatangazwa ambapo utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi mbalimbali utafanyika kuanzia tarehe 9 Agosti hadi 27 Agosti 2025, huku kampeni zikipangwa kuanza tarehe 28 Agosti hadi 28 Oktoba 2025 kwa upande wa Tanzania Bara.
Katika mkutano mwingine na wawakilishi wa wanawake uliofanyika pia jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, amewahimiza wanawake kutumia nafasi zao kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu hatua za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, na kuhamasisha waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Aidha, Jaji Mbarouk ametoa pongezi kwa wanawake kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kilichoanza tarehe 20 Julai 2024 na kukamilika tarehe 4 Julai 2025.
“Natoa pongezi kwenu kwa namna mlivyotuunga mkono wakati wote wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Tunawapongeza na tunawashukuru sana,” alisema Jaji Mbarouk.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa uadilifu, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Natoa wito kwenu kuwahamasisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuepuka mitandao inayosambaza habari za chuki na uchochezi,” amesema Jaji Asina.
“Vilevile, muwakumbushe vijana wenzenu kuepuka matumizi mabaya ya akiliunde. Vijana ni kundi lenye nguvu, na mkitambua nafasi yenu, mtaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” aliongeza.
Katika mikutano yote hiyo, viongozi wa Tume wamekumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika kwa mujibu wa sheria mbili mpya zilizopitishwa mwaka 2024, ambazo zimeleta maboresho ya kiutendaji, kisheria na kiuwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) uliowakutanisha Tume na wawakilishi wa wanawake kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 jijini Dar es Salaam Julai 31, 2025.
Washiriki katika mkutano huo wa wakilishi wa wanawake wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Asina Omari akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) uliowakutanisha Tume na wawakilishi wa vijana kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam Julai 31, 2025.Washiriki katika mkutano huo wa wakilishi wa Vijana wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.
Post a Comment