Header Ads

test

Ithibati yatajwa kuimarisha uaminifu wa Sekta ya Habari na Uchumi wa Vyombo vya Utangazaji

Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesema utekelezaji wa mfumo wa ithibati kwa waandishi na watangazaji wa habari nchini ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha uaminifu, weledi na ushindani wa sekta ya habari katika uchumi wa kisasa unaotegemea taarifa sahihi na zenye kuaminika.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC) uliofanyika Februari 13, 2026 jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema ithibati inalenga kujenga taaluma yenye misingi imara ya kitaaluma, maadili na uwajibikaji kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, ithibati si chombo cha kudhibiti maudhui, bali ni utaratibu wa kuweka viwango vinavyolinda hadhi ya taaluma na kuimarisha imani ya umma kwa vyombo vya habari na kwamba katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kidijitali, uaminifu wa chanzo cha habari ndiyo mtaji mkubwa wa chombo husika.

Ameongeza kuwa vyombo vya utangazaji vinavyowekeza katika weledi wa rasilimali watu wake vinajiweka katika nafasi bora ya kuvutia wawekezaji, matangazo na ushirikiano wa kimataifa, kwa kuwa soko la habari linazidi kuthamini ubora na uwajibikaji.
Kwa upande wa wadau wa mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeelezwa kuwa ushirikiano kati ya msimamizi wa maudhui na wadau wa tasnia ni nguzo muhimu katika kujenga sekta imara, inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hatua ya kuimarisha ithibati inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukuza taaluma za ubunifu na mawasiliano kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa, huku ikihakikisha kuwa sekta ya habari inabaki kuwa mhimili wa uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu.

Waandishi zaidi ya 3,200 kati ya 3,900 walioomba vitambulisho vya uandishi wa habari (Press Card) wamethibitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kisheria, hali inayoonesha mwitikio chanya wa wadau na utayari wa sekta kujiimarisha kitaaluma.

No comments