VIJANA KIBAHA WAPONGEZA HOTUBA YA NANAUKA, WAOMBA USIMAMIZI KATIKA MIKOPO, AJIRA NA MFUMO WA PORTAL
Mwamvua Mwinyi, Kibaha April 22,2026
Baadhi ya vijana wameeleza kuwa licha ya Serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya vijana kwa mwaka 2025/26 pamoja na mpango na makadirio ya matumizi ya mwaka 2026/27, bado changamoto za ajira na upatikanaji wa fursa zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.
Aidha wamempongeza Waziri wa Vijana Joel Nanauka kwa hotuba yake huku wakimuomba kufika Mkoani Pwani ili kusikiliza kero za vijana na kuzipatia ufumbuzi na kuweka utaratibu rafiki wa upatikanaji wa ajira na mikopo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti April 20- 21,2026 katika mbio za mwenge wa Uhuru wilayani Kibaha, baada ya wasilisho la hotuba hiyo Halima Ramadhani, Jamila Jafari, Isack Issa na Emmanuel John walisema changamoto za ajira na upatikanaji wa fursa zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.
Walieleza wimbi la vijana wasomi kukaa bila ajira kwa muda mrefu linaongezeka, huku mfumo wa ajira wa portal pamoja na vigezo vya taasisi za serikali kama TAKUKURU, Polisi na Uhamiaji ukitajwa kutowasaidia ipasavyo.
Mkazi wa kata ya Kawawa Isack Issa alieleza, kuna vijana waliomaliza vyuo kwa zaidi ya miaka nane hadi kumi lakini bado hawajapata ajira, licha ya kuendelea kuomba kupitia mfumo huo na kuitwa kwenye usaili mara kadhaa bila mafanikio.
“Unakuta mtu anaenda kwenye usaili mara tatu au nne lakini hapati kazi, halafu anachukuliwa aliyehitimu hivi karibuni wakati kuna waliokaa nyumbani kwa miaka mingi, Mwisho wa siku kigezo cha umri kinamkuta na anakosa kabisa nafasi,” alieleza Isack.
Aidha, vijana hao walieleza kuwa changamoto ya marefa na ukosefu wa uwazi katika mchakato wa ajira bado ni kikwazo kinachowanyima fursa vijana wengi wenye sifa.
Kwa upande wa mikopo, Juma Amiri, mkazi wa Loliondo Kibaha, alisema licha ya Serikali kueleza kuwepo kwa mikopo ya asilimia 10 na fedha za uwezeshaji, bado vijana wengi hawanufaiki kutokana na masharti na ukosefu wa taarifa kwa wakati.
Naye Emmanuel John alieleza licha ya Mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi, vijana wenye sifa hawapati ajira, akisisitiza kuwa ajira za viwandani zinapaswa kutangazwa kwa uwazi kama zilivyo ajira za serikali na taasisi zake.
Kwa upande wake, Halima Ramadhani alisisitiza haja ya Serikali kuboresha mifumo ya ajira, kuangalia upya vigezo vya umri na kuongeza uwazi katika mchakato wa ajira pamoja na kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia walengwa kwa urahisi.
“Kuna haja ya Serikali kuunda tume maalum ya kushughulikia changamoto za ajira na mikopo ya vijana, pamoja na kupitia vigezo vya taasisi binafsi ili kubaini kwanini fursa zipo lakini bado kuna vikwazo,” alibainisha Halima.
Hata hivyo, katika mkakati wa Serikali wa kuvutia uwekezaji na kuzalisha ajira, Mkoa wa Pwani uliibuka kinara kitaifa kwa kuzalisha ajira 86,621, hatua iliyomfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuipongeza kwa utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa.
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za nguvu kazi, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 12.2, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto hiyo licha ya uwepo wa fursa mbalimbali za kiuchumi.
Akiwasilisha hotuba yake, Waziri anayesimamia maendeleo ya vijana, Joel Nanauka, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo, akieleza kuwa pamoja na ukubwa wa nguvu kazi ya vijana nchini, bado wanakabiliwa na ukosefu wa ajira.
Alifafanua kuna tatizo la kutokidhi ujuzi unaohitajika sokoni, hali inayochangia baadhi ya vijana kushindwa kupata ajira.
Kuhusu mikopo, alisema Serikali imepokea jumla ya Sh bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sekta mbalimbali, na tayari maombi zaidi ya 30,000 yamepokelewa na yanaendelea kuchambuliwa.
Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza, Sh bilioni 48.6 zimetolewa na zinatarajiwa kunufaisha vijana takribani 10,000, huku jitihada zikifanyika kuhakikisha mifumo ya utoaji mikopo inakuwa na uwazi na kuwafikia vijana wengi .
Kadhalika alisisitiza kuwa Serikali imeanzisha Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa mikopo hiyo.
Waziri huyo aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha sera, mifumo ya ajira na uwezeshaji ili kuhakikisha vijana wanapata fursa stahiki na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
.jpeg)

Post a Comment