Benki ya CRDB yadhamini Mei Mosi 2026, yashiriki kikamilifu
Na Mwandishi Wetu
Njombe. CRDB Bank Plc imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono wafanyakazi na maendeleo ya taifa kwa kudhamini na kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa mwaka 2026 yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Maadhimisho hayo yameongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, yakikusanya mamia ya wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wa maendeleo kwa lengo la kutambua mchango wa wafanyakazi katika kukuza uchumi wa nchi.
Kupitia ushiriki wake, CRDB imeungana na Watanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa kusherehekea nafasi ya wafanyakazi katika kuimarisha uzalishaji, ubunifu na ustawi wa jamii. Benki hiyo imekuwa miongoni mwa taasisi zinazoendelea kusisitiza umuhimu wa mazingira bora ya kazi na uwekezaji katika rasilimali watu kama msingi wa maendeleo endelevu.
Ujumbe wa benki hiyo katika maadhimisho hayo uliongozwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, aliyeambatana na timu ya wataalamu kutoka makao makuu, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na matawi mbalimbali ya mkoani Njombe.

Akizungumza pembeni mwa maadhimisho hayo, Rutasingwa alisema ushiriki wa CRDB katika Mei Mosi unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuthamini wafanyakazi wake na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.
Alibainisha kuwa CRDB imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya wafanyakazi wake kupitia mafunzo endelevu, kuboresha mazingira ya kazi na kutoa motisha mbalimbali zinazolenga kuongeza tija na ubunifu kazini.
“Wafanyakazi ndio injini ya mafanikio ya taasisi yoyote. Ndiyo maana sisi kama CRDB tunaendelea kuhakikisha tunajenga mazingira rafiki yanayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na ubunifu zaidi,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kusaidia juhudi za kukuza uchumi jumuishi unaowanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” ikisisitiza umuhimu wa ajira zenye hadhi, haki na usawa katika kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.
Ushiriki wa CRDB katika tukio hilo umeendelea kudhihirisha nafasi ya sekta ya fedha katika kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku benki hiyo ikiendelea kuwa mshirika muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi imara na shindani.


















Post a Comment