
Manyara. Kampuni ya Mati Super Brands Ltd imeibuka kinara katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa mwaka 2026, baada ya kuonesha ubunifu wa hali ya juu na ushindani uliovutia katika vipengele mbalimbali vya sherehe hizo.
Katika tukio hilo lililofanyika kwa shamrashamra kubwa, kampuni hiyo ilitwaa ushindi wa jumla, ikiibuka bora katika maandamano ya miguu, ubunifu wa magari pamoja na uandaaji wa banda bora, hatua iliyowavutia waamuzi na washiriki wengine.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hizo Mei 1, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, aliipongeza Mati Super Brands Ltd kwa ubunifu na kujituma kwake, akisema imeonesha mfano bora wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa wafanyakazi.
“Tumeshuhudia ushindani wa hali ya juu mwaka huu, lakini Mati wamejitofautisha kwa ubunifu, mpangilio na ujumbe waliouwasilisha. Hii ni ishara ya kampuni inayojali wafanyakazi na maendeleo ya jamii,” alisema Sendiga.
Kufuatia ushindi huo, kampuni hiyo ilikabidhiwa kombe la ubingwa wa jumla pamoja na cheti cha pongezi, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuhamasisha ari ya kazi na ubunifu katika maadhimisho ya Mei Mosi.



Kwa niaba ya kampuni, Afisa Rasilimali Watu wa Mati Super Brands Ltd, Doreen Mushi, alipokea tuzo hizo na kueleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya mshikamano na jitihada za wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kampuni itaendelea kuwekeza katika ubunifu na kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
“Ushindi huu unatupa motisha ya kufanya zaidi. Tutazidi kubuni na kuboresha shughuli zetu ili kuendana na mahitaji ya soko na dira ya maendeleo ya taifa,” alisema Mushi.


Naye Mwenyekiti wa Makampuni ya Mati, David Mulokozi, alibainisha kuwa kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kuzingatia mwelekeo wa serikali wa kuimarisha uzalishaji kupitia teknolojia za kisasa.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo imeanza kuzalisha vifaa vya kisasa ikiwemo ndege nyuki (drones) za kunyunyizia dawa mashambani, hatua inayolenga kurahisisha kazi kwa wakulima, kupunguza gharama na kuongeza tija katika uzalishaji.
“Tunataka kuona mkulima wa Tanzania anatumia teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kipato. Hii ndiyo dira yetu kama kampuni,” alisema Mulokozi.






Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” ikisisitiza umuhimu wa ajira bora na mazingira rafiki ya kazi katika kufikia maendeleo ya muda mrefu ya taifa.
Ushindi wa Mati Super Brands Ltd katika maadhimisho hayo umeendelea kudhihirisha nafasi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi, kuhamasisha ubunifu na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira na maendeleo ya kilimo.
Post a Comment