Header Ads

test

Nchi Zinazolima Tumbaku Zaungana Kulinda Zao Linalochangia Uchumi wa Mamilioni

Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

Tanzania imesisitiza umuhimu wa zao la tumbaku kwa uchumi wa nchi kubwa zinazolizalisha barani Afrika, ikitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda ili kulinda maisha ya mamilioni ya wakulima na kuhakikisha sera za kimataifa kuhusu tumbaku zinazingatia hali halisi ya nchi zinazozalisha zao hilo.

Akifungua mkutano wa nchi zinazolima tumbaku uliofanyika jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema tumbaku inaendelea kuwa zao muhimu la kimkakati kutokana na mchango wake mkubwa katika upatikanaji wa fedha za kigeni, ajira, mapato ya Serikali, maendeleo ya viwanda na kupunguza umaskini.

"Kwa nchi zetu, tumbaku si zao la kawaida bali ni bidhaa ya kimkakati inayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi," alisema Chongolo, akisisitiza kuwa sera za kimataifa zinazoihusu sekta hiyo zinapaswa kuzingatia ushahidi wa kisayansi na tathmini halisi ya athari zake kiuchumi na kijamii kwa nchi zinazozalisha.

Alisema tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara nchini Tanzania, likiwa chanzo cha kipato kwa maelfu ya familia za wakulima, kichocheo cha maendeleo ya maeneo ya vijijini na msingi wa ukuaji wa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao.

Chongolo alisema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya kilimo itaendelea kuwa nguzo ya mageuzi ya uchumi, huku mazao ya kimkakati kama tumbaku yakitarajiwa kuongeza mapato ya mauzo ya nje, ajira na ukuaji wa viwanda.

Aliongeza kuwa zaidi ya wakulima 120,000 waliosajiliwa nchini wanategemea tumbaku moja kwa moja, huku mamia ya maelfu ya wananchi wengine wakinufaika kupitia shughuli za usafirishaji, uchakataji na biashara ya zao hilo.

Katika msimu wa mauzo wa 2024/25, alisema wakulima waliuza kilo milioni 160.9 za tumbaku na kujipatia zaidi ya dola za Marekani milioni 411, jambo linalodhihirisha mchango mkubwa wa zao hilo katika kuongeza kipato cha wakulima na mapato ya fedha za kigeni.

Chongolo alisema umuhimu wa tumbaku hauishii Tanzania pekee, akitolea mfano Malawi ambako zao hilo huchangia takribani asilimia 50 ya mapato yote ya fedha za kigeni, hali inayoonyesha nafasi yake muhimu katika uchumi na maisha ya wananchi wa nchi kadhaa za Afrika.

Alizitaka nchi zinazozalisha tumbaku kuimarisha ushirikiano katika tafiti, matumizi ya teknolojia, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza thamani ya mazao na kuendeleza uzalishaji endelevu ili kuongeza ushindani katika soko la dunia.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wakulima wadogo kupitia upatikanaji wa mitaji, huduma za ugani na masoko, huku akizitaka nchi wanachama kuunganisha nguvu katika kutetea maslahi yao ya pamoja kimataifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Victor Mwambalaswa, alisema mafanikio ya sekta hiyo yanategemea ustawi wa wakulima wa tumbaku.

"Kiini cha juhudi zetu zote ni mkulima wa tumbaku. Maendeleo na uendelevu wa sekta hii yanategemea ustawi wa wakulima wetu," alisema.

Mwambalaswa alisema mkutano huo ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu, kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuimarisha ushirikiano katika mnyororo mzima wa thamani wa tumbaku.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Uratibu, Ugatuzi na Mipango ya Maendeleo katika Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri la Zimbabwe, Dk. Willard Manungo, alisema tumbaku ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa nchi yake.

Alisema Zimbabwe inalenga kuvuna kilo milioni 400 za tumbaku mwaka 2026 kutoka kilo milioni 355 zilizovunwa mwaka 2025, huku sekta hiyo ikiwaingizia wakulima zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka uliopita.

Aliongeza kuwa zaidi ya kaya 135,000 nchini humo zinategemea kilimo cha tumbaku kwa maisha yao, huku Serikali ikitekeleza awamu ya pili ya Mpango wa Maboresho wa Mnyororo wa Thamani wa Tumbaku (2026–2030), unaolenga kuongeza uzalishaji hadi kilo milioni 500, kukuza uchakataji wa ndani, kuongeza thamani ya zao na kuimarisha ushindani katika soko la kimataifa.

Dk. Manungo alisema Zimbabwe pia inawekeza katika uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti, matumizi ya teknolojia za ukaushaji zinazookoa nishati, kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha viwango vya kimazingira, kijamii na utawala bora.

Pamoja na changamoto za ziada ya uzalishaji duniani na kushuka kwa bei, alisema ushirikiano wa karibu kati ya nchi zinazozalisha tumbaku ni muhimu ili kuhakikisha sekta hiyo inabaki kuwa endelevu, yenye ushindani na yenye manufaa kwa wakulima.
Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Daniel Chongolo akipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Victor Mwambalaswa alipowasili kufungua mkutano wa wadau wa tumbaku kutoka kwenye nchi tano za Afrika uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa juma.
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo ma wadau wa tumbaku akielekea ukumbini kufungua mkutano wa wadau wa tumbaku mara baada ya kuwasili.Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof.Peter Msofe na kushoto ni Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Stanley Mnozya.
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa zao la tumbaku kutoka nchi 5 za Afrika mara baada ya kufungua mkutano wao mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam
Wadau wa zao la tumbaku kutoka nchi tano za Africa wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo wakati akifungua mkutano wao uliofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dar ea Salaam

 

No comments