Header Ads

test

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI, MZUMBE WAWASHIKA MKONO WENYE MAHITAJI

Menejimenti na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe wameadhimisha Siku ya Wanawake
Duniani kipekee, ambayo kilele chake ni Machi 8, 2023 kwa kuwatembelea watoto wenye
mahitaji maalumu na wafungwa wanawake katika Gereza la Kingolwira, Mkoani Morogoro.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mwakilishi wa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof.
Allen Mushi, ilifanywa na akinamama wa Chuo hicho Kampasi Kuu, sambasamba na kuwapatia
mahitaji mbalimbali watoto katika kituo cha Amani na wafungwa.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kituo cha Amani kilichopo kijiji cha Magubike Wilaya ya
Mvomero, umbali wa kilomita 75 kutoka Morogoro mjini; Prof Mushi, ameisihi jamii kuendelea
kuyatambua makundi maalum ya Watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu kwani
nao wana haki sawa na watoto wengine na wanastahili elimu na mazingira bora ya kusoma na
kuishi.

Aidha, Prof.Mushi ameipongeza Jumuiya ya wanawake wa Chuo hicho kwa kubuni wazo la
kuwatembelea kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wafungwa, kwakuwa
wameonyesha kwa dhati nafasi ya mama katika malezi ya mtoto na hivyo hawana budi
kuungwa mkono.

“ Sisi tumeamua kuanza mapema kuadhimisha siku hii, ili kutoa fursa kwa wanawake kujiunga
na wengine duniani kote kuadhimisha siku hii ya kipekee tarehe ya kilele tarehe 08 Machi 2023.

Ushiriki wetu hapa leo hii unaonesha ni kwa namna gani tunaiishi Kauli Mbiu “Ubunifu na
Mabadiliko ya Teknolojia ni Chachu katika Kuleta Usawa wa Kijinsia”; kwani wavumbuzi na
wabunifu ni hawa wanafunzi tunao waona mbele yenye, wakipewa nafasi wanaweza. Hii ni
nguvu kazi ya Taifa la kesho, na hawa ni wanafunzi wetu miaka michache ijayo, ndiyo maana
tumeamua kuanza kuwalea, kuwatambua na kuwajali sasa” Alisema.



Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Athumani Mbilikila, ametoa shukrani za dhati kwa Menejimenti
na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuona umuhimu wa kutembelea shule hiyo na
kutoa misaada ya vitu mbalimbali, kwa Watoto wanaoishi kwenye kituo hicho wakitokea
maeneo mbalimbali nchini, na kuongeza kuwa watoto hao wamekuwa wakitegemea kituo hicho
kwa kila kitu kutokana na Wazazi na Walezi kushindwa kumudu gharama; huku shule hiyo ikiwa
inakabiliwa na changamoto nyingi za uendeshaji.

Amesema pamoja na shule hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya darasa la Saba na
Darasa la Nne mwaka 2022, bado kumekuwa na changamoto kubwa ya vifaa vya kujifunzia na
kufundishia vikiwemo vitabu na vifaa maalumu kwa watoto wenye uoni hafifu na wasiosikia.

Awali akisoma risala kwa wageni, Mwl. Sadick Said, Mtaaluma wa shule hiyo alieleza kuwa kwa
sasa shule hiyo inatoa elimu jumuishi kwa walemavu na wasio na ulemavu na ina jumla ya
Wanafunzi 81 kati yao wavulana ni 38 na wasichana 43 na Walimu 12 Wanawake wakiwa 7 na
wanaume 5, huku Watoto wenye ulemavu mbali mbali wakiwa ni 27. Amesema kwa sasa Shule


hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki inatoa elimu kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari,
huku ikiwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa Chakula, vifaa vya kufundishia, uhaba wa
walimu na miundombinu chakavu.

Katika ziara hiyo, jumla ya vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Tshs mil 4 vilitolewa ikijumuisha
bidhaa za chakula (unga, mchele, sukari, mafuta ya kupikia,,maharage, juice na biskuti), taulo la
kike, sabuni, miswaki na dawa, kandambili na nyinginezo. Vifaa hivyo vilitolewa kwa watoto wa
shule ya Amani na wafungwa wa kike katika Gereza la Kingolwira.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ameahidi kupeleka Televisheni katika shule hiyo
ili kuwawezesha Wanafunzi kutazama taarifa baada ya muda wa masomo.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Allen Mushi akisaini kitabu cha Wageni baada ya
kuwasili shule ya Elimu Maalum Amani, iliyopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Baadhi ya Watoto wa shule hiyo wakiwakaribisha Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa wimbo
maalum.
Mkuu wa shule ya Elimu maalum ya Amani , Mwl. Athumani Mbilikila akisoma hotuba yake na kutambulisha wa wageni kwa Wanafunzi na Wafanyakazi wa shule hiyo.
Mwalimu wa Taaluma wa shule ya Amani Sadick Said akisoma risala.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha na Utawala
akitoa salaam kwa niaba ya Wafanyakazi wa Chuo kwa Wanajumuiya ya shule ya Amani.
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Walimu na Wanafunzi wa shule ya Amani wakifuatilia hafla ya
kukabidhi mahitaji
Menejimenti na Wafanyakazi wa Chuo kikuu Mzumbe wakiwagawia zawadi mablimbali kwa Watoto wa Shule Maalum ya Amani.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Allen Mushi (kulia) na Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Dkt.Harold Uttoh (kushoto) wakikabidhi rasmi mahitaji ya Watoto kwa Mkuu wa Shule yaAmani Mwl.Athumani Mbilikila (katikati)
Wafanyakazi wa Chuo kikuu Mzumbe na Wanafunzi wa shule ya Amani katika picha ya pamoja.
Wawakilishi wa wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakikabidhi vifaa kwa wafungwa wanawake katika gereza Kingolwira, Morogoro

No comments