Header Ads

test

MFUKO WA SELF WAMWAGA MIKOPO YA BILIONI 313 KWA WANUFAIKA 225,000 NCHINI

 

 

Meneja Masoko na Uhamasishaji wa mfuko wa Self Mirofinance Fund, Linda Mshana, akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu shughuli zinazofanywa na SELF MF katika kukuza uchumi kwa Wananchi. 

Na Dotto Mwaibale, Dodoma 

MFUKO wa  SELF MICROFINANCE FUND uliopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ambao una jukumu la kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wenye kipato cha chini umetoa mikopo ya Sh.bilioni 313 kwa wanufaika 225,000.

Meneja Masoko na Uhamasishaji wa mfuko huo, Linda Mshana, akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu shughuli zinazofanywa na SELF MF katika kukuza uchumi kwa Wananchi alisema mikopo hiyo imetolewa katika kipindi cha kuanzia 2000 hadi 2022.

Alisema mikopo hiyo yenye masharti nafuu imetolewa kwa wajasiriamali wadogo, taasisi za fedha,benki za kijamii na Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na kwamba mfuko ulianza na mtaji wa Sh.Bilioni 62 lakini kutokana na marejesho mazuri kutoka kwa wakopaji ambayo ni takribani asilima 93 mtaji wa mfuko umefikia Sh.bilioni 313 ambazo zimekopeshwa kwa wajasiriamali.

Mshana alisema mikopo hiyo inayo lenga kuwapa watu fursa ya kufanya shughuli za uzalishaji mali itasaidia kukidhi mahitaji ya kifedha kwa makundi mbalimbali ya watu wakiwamo wakulima, wafugaji na wafanyabiashara.

“Moja ya jukumu letukubwa  ni kuwapa watu fursa ya kufanya kazi kwa kutoa huduma ndogo za fedha kwa masharti nafuu na kuwa jambo la msingi kwa wakopaji wanatakiwa kuwa waadilifu, wenye umoja, wabunifu na wawajibikaji katika kujiletea maendeleo endelevu,” alisema Mshana.

Aziza Nasibu ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mfuko huo alisema anaushukuru Mfuko wa Self Microfinance kwani umesaidia kuongeza mtaji wa biasharayake.

Aziza ambaye anamili Kiwanda cha Cal Plastick mjini hapa ambacho kinachakata makopo hususan ya maji,alisema mfuko huo ulimkopesha sh. Milioni 50 ambazo zilisaidia kuinua kiwango cha biashara yake.

Mnufaika mwingine wa mfuko huo Wema Sehaba ambaye anafanya bishara ya kuuza pembejeo za kilimo alisema mfuko huo umemkopesha Sh.milioni 40 ambazo zimemsaidia kukuza mtaji wa biashara yake.

Wema alisema miezi miwili ijayo atakuwa amemaliza kurejesha marejesho ya mkopo huo wa awali na kwamba anatarajia kukopa Sh.milioni 80 ambazo pamoja na mambo mengine atafungua maduka ya pembejeo za kilimo nje ya mkoawa Dodoma.

Meneja wa Tawi la Dodoma, Aristid Tesha, amesema mikopo inayotolewa na mfuko huo inakuwa na bima isipokuwa ile inayotolewa kwa kampuni na kwamba bima inayotozwa kwa mteja ni asilimia 0.6 kwa mwaka na inamsaidia mteja anapopatwa na majanga na kukwama kurejesha mkopo wake.

Tesha, alisema ofisi yao ya Dodoma ipo Makaru njia pada ya kwenda majumba sita kushoto linaonekano bango kubwa na kulia kuna kituo cha bodaboda.

Meneja wa Tawi la Dodoma, Aristid Tesha, akizungumza katika mafunzo hayo.
Mwanahabari Getrude akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.


Meneja wa Tawi la Dodoma la mfuko huo, Aristid Tesha, akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo. Kushoto ni  Meneja Masoko na Uhamasishaji wa mfuko huo, Linda Mshana.

Mafunzo yakitolewa.
Mnufaika wa mfuko huo Aziza Nasibu akizungumza na waandishi wa habari.
Ziara ya kutembelea kwa mnufaika wa mkopo kutoka mfuko huo, Aziza Nasibu ikifanyika.

Ziara ya kumtembelea mnufaika wa mfuko huo, Aziza Nasibu ikifanyika.
Mnufaika wa mkopo kutoka katika mfuko huo, Wema Sihaba akizungumzia mafanikio aliyopata baada ya kupata mkopo kutoka katika mfuko huo.

Muonekano wa ofisi ya mfuko huo iliyopo Dodoma eneo la Makuru njiapanda ya kwenda majumba Sita Barabara kuu ya kwenda Chuo Kikuu cha UDOM.

No comments