Header Ads

test

MAWAKALA WA FORODHA WAHIMIZWA UDHIBITI WA KEMIKALI HATARISHI

Serikali imewataka mawakala wa forodha wanaoandaa nyaraka za kuingizia nchini na kupokea
mizigo ikiwemo kemikali zinazodhibitiwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo
zinazochangia mmong’onyo wa tabaka la ozoni na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Wito huo umetolewa Machi 1, 2023) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Catherine Bamwenzaki wakati akifungua
mafunzo kwa mawakala wa forodha kuhusu udhibiti na usimamizi wa kemikali na vifaa vya
kemikali vinavyomong’onyoa tabaka la ozoni.

Amebainisha kuwa kemikali au gesi zinazotumika katika mojokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia
moto, usafirishaji chuma, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kuwa iwapo hatua
hazitachukuliwa zinaweza kuingizwa nchini kupitia mipaka na kusababisha madhara kwa
binadamu na mazingira.

Mhandisi Bamwenzaki amesema uchunguzi wa angahewa uliofanywa na wanasayansi
umethibitisha kuwa Tabaka la Ozoni limekuwa likimong'onyoka kwa kasi ya asilimia tano (5) kila
muongo ambapo matokeo ya uharibifu huo ni pamoja na kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani
kufika katika uso wa dunia.

Akifafanua zaidi Mhandisi Bamwenzaki amesema matokeo ya uvumbuzi huo yalisababisha
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kufanya tathimini ya kisayansi na kuamua
kuchukua hatua madhubuti katika kulinda tabaka hilo la Ozoni.

“Chini ya Programu ya Taifa, Serikali imeandaa na inatekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali
Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni ifikapo mwaka 2030 ambapo moja ya shughuli
zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa elimu kwa mawakala wa forodha na wasimamizi wa Sheria
kuhusu Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2022” amesema Mhandisi Bamwenzaki.

Akiwasilisha Mada kuhusu Udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiewa chini ya Itifaki ya
Montreal, Afisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi George Ngoso
amesema suala udhibiti wa kemikali na vifaa vya kemikali linahitaji nguvu ya pamoja vaina ya
wadau waliopo katika mnyororo wa thamani ili kulinda afya za binadamu na mazingira.

Mhandisi Ngoso amesema ni wajibu wa mawakala wa forodha waliopo mipakani kujifunza
teknolojia mpya ya ukaguzi wa mizigo ikiwemo bidhaa za kemikali kuendelea na usimamizi na
udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.
“Mnapaswa kuwa wazalendo na kutanguliza maslahi ya taifa na jamii inayowazunguka,
madhara ya uingizaji wa bidhaa hizi unaweza kuleta athati kuwa kwa afya za binadamu na
mazingira, hivyo tunapaswa kuhakikisha kuwa tunadhibiti kemikali hizi kutoweza kuingia katika
jamii yetu” amesema Ngoso.

Kwa upande wake Wakala wa Forodha kutoka Kampuni ya Freight Forwarders James Mramba
ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha mafunzo hayo na kusema yataongeza
tija katika utekelezaji wa majukumu yao sehemu za kazi na kuhimiza mafunzo hayo kuwa
endelevu ili kuwafikia wanufaika wengi zaidi.

“Naahidi kuwa Balozi kwa wenzangu kwa kushirikiana na watumishi wenzangu pamoja na
taasisi nyingine za serikali ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na udhibiti wa kutosha wa uingizaji
wa kemikali ambazo zina athari kubwa kwa jamii na mazingira yetu” amesema Mramba.

Katika mafunzo hayo washiriki hao walielimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira
(Kanuni za Kudhibiti Kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022, Udhibiti wa
Uingizaji wa Kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itikafi ya Montreal, na Taratibu za maombi ya
vibali vya usimamizi wa kemikali.

Jumla ya Mawakala wa forodha 25 walishiriki mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Machi 01
hadi 03, 2023 na kuandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mhandisi Goodluck Rulagora kutoka Chuo cha Uvuvi Bagamoyo (FETA) akitoa ufafanuzi
kuhusu matumizi ya vipimo sahihi vya kemikali vinavyotumika katika vifaa mbalimbali ikiwemo
mitungi ya gesi kwa mawakala wa forodha wakati wa mafunzo ya siku. Mafunzo hayo
yanaendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku ya mbili kwa Mawakala wa Forodha wanaohusika na
udhibiti na usimamizi wa kemikali na vifaa vya kemikali vinavyomong’onyoa tabaka la ozoni.
Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Taasisi za Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) Jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

No comments