Header Ads

test

Muhimbili Yaandaa kongamano la siku mbili la Saratani

 

Na Mwandishi Wetu

Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa kongamano la siku mbili la saratani ya ini Tanzania kuanzia Machi 17 hadi 18, 2023 lenye lengo la kujadili jinsi ya kuunganisha nguvu ya kupambana na Saratani ya Ini nchini ili kuipunguzia serikali mzigo wa matibabu kwa wananchi wanaokumbwa na ugonjwa huo.

Akizungumza na vyombo vya habari Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH Dkt. John Rwegasha amesema majadiliano ya kongamano hilo yanalenga kuboresha huduma kwa walio katika hatari na waliokwisha ambukizwa na pia kuihamasisha jamii kupambana na saratani ya ini.

Dkt. Rwegasha ameongeza kuwa ugonjwa wa Saratani ya Ini unachukua nafasi ya sita Duniani katika vifo vyote vinavyosababishwa na magonjwa ya Saratani kwa makadirio ya vifo 780,000 ambapo asilimia 80 wanatoka nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia.

“Tafiti zinaonesha kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara Saratani ya Ini hujitokeza katika umri mdogo kwa wastani wa kuanzia umri wa miaka 30, hata hivyo kupitia juhudi mbalimbali za Serikali, Hospitali ya Muhimbili inatoa huduma za matibabu nchini kwa kuwa kuna wataalamu waliobobea na vifaa tiba vya kuwezesha kutolewa kwa huduma hiyo” ameongeza Dkt. Rwegasha

Dkt. Rwegasha amebainisha kuwa Muhimbili inatoa matibabu ya kisasa kwa njia ya tiba Radiolojia (Intervention Radiology) ya kutoa dawa moja kwa moja kwenye uvimbe kupitia mirija ya damu, matibabu ambayo awali yalikuwa hayapatikani nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kongamano la Saratani ya Ini Tanzania, Dkt. Ally Mwanga amesema kongamano hilo limetanguliwa na upimaji na matibabu ya Homa Ini bila malipo kuanzia Machi 16 hadi 17, 2023 ambapo takribani watu 684 wamepimwa na kati ya hao 30 wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. John Rwegasha akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Kongamano la Saratani.

No comments