Header Ads

test

MTOTO APOTEA HIFADHINI APATIKANA BAADA YA SIKU MBILI




Na Mwandishi Wetu.

MTOTO anayefahamika kwa jina la Justin Kiluso(5) amenusurika kuliwa na wanyama wakali baada ya kupotea katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa siku mbili alipokuwa akichunga ng'ombe na wenzake katika kijiji cha Kakoyi kilichopo jirani na hifadhi hiyo.

Mtoto huyo alipotea Jumapili ya Pasaka ya tarehe 9 ya mwezi huu majira ya mchana hifadhini humo ambapo alipatikana Jumanne siku mbili baadaye akiwa na hali mbaya kiafya kutokana na kukosa chakula kwa siku zote hizo.

Hayo alibainika juzi baada ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira(JET) kutembelea Jumuia ya Hifadhi ya Burunge kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID unaolenga kulimalisha uhusiano mwema kati ya binadamu na wanyamapori katika shoroba ya Kwakuchinja.

Akieleza juu ya mkasa huo Mwenyekiti wa kijiji cha Kakoyi Loiseye Elias alisema alipokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo jioni baada baada ya wazazi wake kurudi nyumbani kutoka mnadani na kuambiwa mtoto wao haonekani tangu mchana.

Elias alisema siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni Jumatatu walipiga mbiu na wanakijiji kutoka vijiji vinne vya Mswaki,Olasiti,Minjingu na Kakoyi walikusanyika na waliingia porini na kuanza kumsaka mtoto huyo bila mafanikio.

"Watu zaidi ya 500 waliingia porini kumtafuta mtoto huyo,tulipata msaada wa magari kutoka kwa mwekezaji kampuni ya Chemchem lakini hatukuweza kumuona hivyo tulendekea kumsaka hadi tukafika kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire"alisema Elias.

Mwenyekiti huyo alisema walianza kumsaka kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa mbili usiku ambapo alieleza kuwa waligundua kuwa update walioelekea ulikuwa tofauti na kule alipokuwa mtoto.

Alisema siku iliyofuata yaani Jumanne walipigiwa simu kujulishwa mtoto huyo amepatikana kwani aliokotwa na askari wa wanyama pori akiwa ameishiwa nguvu kutokana na kukosa chakula.

"Tunamshukutu Mungu kwani maeneo aliyopita ni hatari kutokana na kuwa na wanyama wakali na kwamba askari hao walituambia kuwa mita 200 kutoka pele walipokutwa mtoto huyo kulikuwa na kundi la simba"alisema Elias.

Kiongozi huyo wa kijiji alisema baada ya kupatikana alipatiwa uji kama huduma ya kwanza na kisha kupelekwa kituo cha afya cha Ngaiti na ilibainika kuwa sukari yake imeshuka.

Aidha alisema kuwa matukio kama hayo yaliwahi kutokea miaka ya nyuma na kwamba la hivi karibuni lilitokea tukio kama hilo mwaka 2020 ambapo mtoto wa miaka saba naye alipotea lakini alipatikana siku hiyo hiyo.

"Mbali na kudra za Mwenyezi Mungu lakini pia kilichomsaidia mtoto huyu kutolaluliwa na wanyamapori ni kwa sababu tumezoeana kwani hata huko machungani tumekuwa tukipichana nao hivyo huwenda wanyama hao walimuona lakini wakaendelea na mambo yao"alisema Elias.

Kauli za baba mzazi.

Akieliza hali ya mwanaye baba mzazi wa mtoto huyo Semari Kiluso alisema waliruhusiwa kutoka hospitalini Alhamis iliyopita na mtoto wake anaendelea kunywa dawa alizopatiwa na wataalamu wa kituo hicho cha afya.

Alisema mwanaye alimweleza kuwa alikutana na fisi lakini alimtishia kwa fimbo hali iliyopolekea fisi huyo kukimbia na pia alisema kuwa aliwaona simba wakipita lakini hawakumfanya kitu.

Mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori katika hilo umetajwa kwamba umekuwa mzuri kwa kipindi kirefu na hii ni kwa sababu wanaishi vizuri na wanyama hao na hata wanapovamia makazi ya watu wamekuwa hawasababishi madhara makubwa.

Kwa upande wake Chifu wa kabila la Wamasai katika kitongoji cha Eluwayi kilichopo katika kijiji cha Olasiti,Leteiva Loburu alisema kuwa simba wa Tarangire siyo wachokozi ukilinganisha na wale wa Manyara.

Alisema kwamba mnyama mkorofi ni fisi ambao wamekuwa wakifanya uharibifu pale wanapoingia kwenye maboma ya mifugo(zizini) hasa la mbuzi na kondoo.

"Kuna siku fisi akiingia zizini na kuua mbuzi 24 na hakula hata mmoja kwani baada ya kuua idadi ya mbuzi hao aliondoka na kwenda zake porini"alisema Loburu.

Aidha kiongozi huyo wa kilimila alisema kuiwa siku hizi ushujaa wa kijana wa kimasai siyo kuua simba kama ilivyokuwa hapo awali na hii ni kutokana na wengi kupata elimu iliyosaidia vijana hao kubadili tabia zao na kuwaona wanyama hao kama rafiki zao wanaohitaji kutunzwa na siyo kuwindwa.

No comments