Header Ads

test

TAMICO YAENDELEA KUWA MFANO WA KUIGWA NDANI NA NJE YA NCHI

 

Ufanisi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Wizara ya Madini kwa ujumla waivutia Kenya na kuifanya kuja Tanzania kujifunza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uchimbaji madini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Uchumi wa Bluu nchini Kenya Elijah Mwangi wakati wa ziara yake ya wiki moja akiambatana na ujumbe wa wataalamu sita kutoka nchini humo waliokuja kujifunza na kuona jinsi STAMICO na Wizara ya Madini kwa ujumla wanavyofanya shughuli zake .

Mwangi ameipongeza STAMICO na kusema kuwa imekuwa ikifanya vizuri katika kuendeleza shughuli za mnyororo wa thamani wa uchimbaji madini hivyo wataendelea kujifunza kwa namna ambavyo imefanikiwa katika kuendesha shughuli za madini zikiwemo utafiti, uchimbaji, uchakataji, na biashara ya madini

Amesema anaamini kuwa kwa sasa Tanzania inanufaika vya kutosha kutokana na rasilimali hizo kupitia sheria na taratibu zilizowekwa.

“Tumejifunza mambo mengi kwa jinsi gani madini yanaweza kubadilisha maisha ya wanajamii na Taifa kwa ujumla, tumekuja hapa ili kuweza kujifunza, kwa sababu sisi bado ni Shirika changa ambalo hatuwezi kujilinganisha na STAMICO ambalo limeanza muda mrefu, na hatukuona sababu ya kuchagua nchi nyingine kwaajili ya kujifunza isipokuwa Tanzania, tunashukuru sana kwa kuwa majirani wema na kufungua milango kwaajili yetu.” Amesema Mwangi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amefurahishwa na ujio wa ujumbe huo ambao umeona ni vyema kujifunza kutoka Tanzania juu ya shughuli za uchimbaji na usimamizi wa rasilimali madini, huku akiamini kuwa ushirikiano huo utasaidia kukuza diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo.

“Tumejadiliana mengi na tumebadilishana uzoefu wa namna ya kuendesha Sekta ya Madini, nini kinatakiwa kufanyika hasa kwenye maeneo ya masoko, kuwawezesha wachimbaji wadogo na usafishaji wa Madini ili kuhakikisha maslahi katika shughuli yoyote inayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa madini inasaidia kuleta mabadiliko kwenye sekta ndogo ya uchimbaji sambamba sekta zingine

" Taifa lenye rasilimali linatakiwa kushiriki kikamilifu kwenye uvunaji wa rasilimali hizo, wameona sisi tumefanya vizuri kwenye maeneo hayo na wamekuja kujifunza, tumewaelezea namna tunavyonufaika na asilimia kumi na sita za hisa za serikali kwenye migodi, tumeeleza pia namna ambavyo Shirika hili la Taifa linanufaika kutokana na hii Sekta ya Madini" Alisema Mwasse.

Mwasse amesema kuwa watahakikisha wanawatembeza wageni hao katika maeneo mbalimbali ya Shirika hilo ili wajionee namna ambavyo shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa vitendo, huku akisema kuwa wataweka msingi mzuri wa ushirikiano.

“Geolojia haina mipaka, lakini nchi ndiyo zenye mipaka kinachopatikana huku huenda kinapatikana pia kule Kenya, kwahiyo sisi tuko tayari kushirikiana nao kwenda kule kuwasaidia kugundua na kuweza kuona ni namna gani wanaweza wakasimamia rasilimali hizo ili ziweze kunufaisha watu wao.”

Ziara hiyo itahusisha mafunzo sambasamba na kutembelea baadhi ya maeneo ya migodi yakiwemo vituo vya mfano vya uchimbaji mdogo, kiwanda cha kusafisha dhahabu na Mgodi wa STAMIGOLD unaomilikiwa na Serikali.








No comments