WAZALISHAJI MBOLEA NA VISAIDIZI VYA MBOLEA NCHINI WATAKIWA KUZINGATIA VIWANGO VYENYE UBORA
Na Mwandishi wetu
Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewataka wazalishaji wa ndani wa mbolea na visaidizi vya mbolea kuzingatia ubora wa bidhaa zao kabla hawajazipeleka sokoni ili kulinda afya za watumiaji wa bidhaa hizo.
Wamesema ili mbolea ipate kibali cha kuuzwa ndani na nje ya nchi ni lazima iwe na vyeti vinavyothibitisha ubora wa bidhaa kutoka Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) lakini pia vibali vyote kutoka mamlaka zinazosimamia tasnia hiyo.
Aidha, iwe imekidhi matakwa ya sheria ya Mbolea inayosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA pamoja na matakwa ya mamlaka nyingine kama kama vile Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mkemia Mkuu wa Serikali na nyinginezo.
Wametoa kauli hiyo nyakati tofauti walipofanya ziara kwenye viwanda vinavyozalisha mbolea na visaidizi vyake katika mikoa ya Dar Es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ikiwa ni ziara iliyolenga kujifunza pamoja na kuwahamasisha kuongeza uzalishaji wa bidhaa wanazozalisha hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika kikao baina ya wajumbe wa bodi, Menejimenti ya TFRA na Menejimenti ya kiwanda cha Minjingu jana tarehe 21 Julai, 2023, Mkurugenzi wa Bodi, Thobias Mwesiga amewataka wamiliki wa kiwanda hicho kuwa na ubora usioteteleka katika bidhaa zao ili kuepusha malalamiko yatokanayo na ubora wa bidhaa hizo pindi zinapotumika kwenye kilimo.
Pamoja na hilo akizungumza katika kiwanda cha mbolea za maji cha keenfeeder aliwataka wawekezaji hao kuzoea kukaguliwa na mamlaka kwani jukumu hilo ni endelevu katika kuhakikisha viwango vilivyokubaliwa ndivyo vinavyoingizwa sokoni.
“Suala la ukaguzi wa mbolea linalofanywa na TFRA lizoeeni maana litafanyika sana” Mwesiga alikazia.
Kwa upande wake Hadija Jabiri aliwataka wawekezaji hao kuona namna wanavyoweza kuwasaidia wakulima kutambua afya ya udongo kabla ya kutumia bidhaa zao ili kutumia bidhaa zinazoendana na aina ya virutubisho vinavyohitajika kwa mmea katika maeneo yao.
Aidha, aliwataka wawekezaji hao kutosita kueleza changamoto wanazokutana nazo kwenye shughuli zao za uzalishaji kwani Bodi ya Wakurugenzi wakishirikiana na Menejimenti ya TFRA kama wasimamizi wa tasnia wanaweza kushauri namna bora ya kuendeleza na kutatua changamoto zao.
Akiwashauri juu ya changamoto ya mitaji iliyowasilishwa kwa takribani wazalishaji wote waliotembelewa, Hadija alishauri kuandaa maandiko na kuwasilisha kwa taasisi mbalimbali za kimataifa zinazotoa misaada kwa wajasiliamali na kueleza hatua hiyo itasaidia sana katika kupunguza changamoto hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi, Lilian Gabriel alitamani kujua mbinu zinazotumiwa na wazalishaji katika kuhakikisha ubora wa bidhaa wanazozalisha na kuelezwa kuwa, ubora wa bidhaa zinazozalishwa hususani kwa kiwanda cha Minjingu unaanzia kwenye malighafi zinazotumika kuzalishia mbolea zao ambapo ni lazima zikidhi viwango ndipo zikatumike kwenye uzalishaji.
Akieleza hayo, Mtendaji Mkuu wa Kampuni la Minjingu, Mahesh Kumar Parik ameeleza kuwa kiwanda chao kina maabara inayowawezesha kuchukua sample kwa kila kilichozalishwa na kupima kabla ya kukipeleka sokoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Josepy Charos alisema serikali ilitumia kiasi cha shilingi Bilioni 700 kuagiza mbolea nje yan chi ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini.
Alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kuwataka wazalishe kwa wingi ili fedha inayotumika kuagiza mbolea hizo nje ifanye shughuli nyingine za maendeleo nchini.
Kwa upande wa menejimenti za vilivyotembelewa vilieleza kufarijika sana kutokana nah atua iliyochukuliwa na bodi Kwenda kuwatia moyo na kusikiliza changamoto zao lakini pia kuwashauri njia bora za kuendeleza shughuli zao.
Naye Alfred Masawe kiwanda cha mbolea za maji cha keenfeeder alikiri kuwa TFRA kwa sasa inafanya kazi kama mlezi na mshauri tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma i na kukiri ushirikiano wanaopewa ni mkubwa unaowawezesha kusonga mbele katika uzalishaji wa mbolea za maji.
Katika ziara hiyo ya siku 5 wajumbe wa bodi ya TFRA walitembelea kiwanda cha Neelkanth Chemicals LTD, kiwanda cha ABM vya mkoani Tanga, kiwanda cha mboji cha Mkoani Kilimanjaro, Keenfeeder, Agri farmers, Sianga, Mtali vya mkoani Arusha na kiwanda cha Minjingu kilichopo mkoani Manyara.
Post a Comment