Header Ads

test

HUYU HAPA DKT. SLAA ALIYEVULIWA UBALOZI

Na Mwandishi Wetu

Mnamo Septemba mosi, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemvua hadhi ya Ubalozi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt. Willibrod Peter Slaa ambaye aliteuliwa kwenye nafasi hiyo Novemba 2017 hadi Septemba 2021.
Dkt. Slaa aliteuliwa kwenye nafasi hiyo na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Akiwa katika kituo chake cha kazi mjini Stockholm, Sweden, Dkt. Slaa aliidhinishwa pia kwenye nchi za Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Ukraine na Lithuania.

Mwanasiasa huyo mkongwe kwenye taifa la Tanzania, alizaliwa Oktoba 29, 1948. Dkt. Slaa aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Jimbo la Karatu.

Dkt. Slaa pia alikuwa Mwanachama mkongwe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akihudumu kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama (1998 hadi 2002) sanjari na kuhudumu kwenye nafasi ya Katibu Mkuu.

Dkt. Slaa ni msomi wa Shahada ya Juu (PhD) ya masuala ya Sheria ambayo aliipata kwenye Chuo Kikuu cha St. Urban mjini Rome, nchini Italia, mnamo mwaka 1977.


Awali, Dkt. Slaa alipata elimu yake katika Shule ya Seminary ya Kipalapala iliyopo mkoani Tabora kabla ya kupata elimu ya masuala ya dini, ngazi ya cheti mwaka 1977. Aidha, Dkt. Slaa alipata elimu kwenye Shule ya Seminary ya Kibosho, ngazi ya cheti akisoma masuala ya Falsafa.

Pia, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye Mashirika mbalimbali nchini Tanzania, mwaka 1985 hadi 1991 alikuwa Katibu Mkuu wa ‘Tanzania Episcopal Conference (TEC), miaka 1982 na 1985 alikuwa Mkurugenzi wa Dayosisi ya Maendeleo ya Mbulu.

Vile vile, Dkt. Slaa alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ‘Tanzania Society for the Blind (TSB)’ kati ya mwaka 1992 hadi 1998.

No comments