KAMISHNA ARDHI SINGIDA ATOA ONYO KAMPUNI ZA UPIMAJI ZITAKAZOTOZA BEI ISIYO ELEKEZI
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, akizungumza katika kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi kilichofanyika Septemba 1, 2023 mkoani Singida.
...................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida.
KAMISHNA wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, ametoa onyo kwa
makampuni ya upimaji ardhi mkoani hapa kuhakikisha yanatoza bei elekezi
iliyopangwa na Serikali wakati wa upimaji ardhi kinyume na hapo yatachukuliwa
hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa kibali cha kufanya kazi
hiyo.
Hoza, ameyasema hayo Septemba 1, 2023 katika kikao kazi cha watumishi wa
sekta ya ardhi na kueleza kwamba kampuni zinazojishughulisha na upimaji ardhi
zisijiingize kutoza fedha nyingi kinyume na maelekezo ya serikali kwani kufanya
hivyo ni kudhoofisha jitihada za Serikali ambayo inataka kuhakikisha kila
mwananchi anamilikishwa ardhi kwa ajili ya maendeleo na kwamba kampuni
itakayobainika inaongeza bei hizo itachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo
kufungiwa kufanya kazi hiyo mkoani Singida.
‘’ Kampuni itakayobainika kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa kwa mujibu
wa sheria kwa kutoza bei kubwa ya upimaji tofauti na ile iliyopangwa na
Serikali unajulikana wazi na hatua kali
itachuliwa ikiwa kufutiwa usajili pamoja na kuzuiliwa kufanya kazi hiyo,’’
alisema Hoza.
Alisema lengo la Serikali kushirikiana na taasisi na makampuni binafsi ni
kusogeza huduma na kuhakikisha wananchi wanazipa kwa urahisi hivyo haiwezi
kuvumilia kuona wananchi wake wakifanyiwa ndivyo sivyo.
Aidha,Hoza amewaomba Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa
kushirikiana na kampuni hizo na kuwa uwezo wa Serikali wa kupima maeneyo yote
kwa wakati mmoja ni kazi ngumu na kuwa maendeleo ya wananchi yanakwenda kwa
kasi hivyo aliomba makampuni hayo yapewe ushirikiano na kuhakikisha maeneo yote
yanapangwa kwa kupimwa na kumilikishwa jambo litakalo saidia kuondoa makazi
holela na kuifanya miji kupangika vizuri.
Afisa Ardhi Wilaya ya Manyoni, Pendo Mwakila,alisema lengo la kikao hicho ni
kuwataka maafisa ardhi kutoka ofisini na kuwafuata wananchi waliko ili kusikiliza
kero zao ili kuwapunguzia gharama za kuwafuata maofisini na kuwa wao walikwisha
anza katika Kata za Kintiku na Kilimatinde.
Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini ]TAKUKURU], mkoani hapa, Shemu Mgaya akitoa
mada katika kikao hicho alizungumzia kuhusu maadili ya utumishi wa umma na
watumishi wakiwamo wa sekta ya ardhi kutojihusisha na rushwa katika utendaji wa
kazi zao.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida, Bahati Colex aliwaomba
maafisa ardhi kushirikiana na wananchi wanaoshinda kesi kurudishiwa maeneo yao
kwani imekuwepo changamoto kubwa kutoka kwa maafisa hao ya kuwazungusha pasipo
sababu yoyote licha ya kushinda kesi hizo.
‘’ Inapofikia hatua sasa ya kurudishiwa hivyo viwanja kunakuwa na
uzungushaji mwingi kiasi kwamba mtu husika anakuwa kama anaanza kesi upya
niwaombe tushirikiane katika eneo hilo hasa kwa wale ambao wanahusika
kutekeleza amri za mahakama inafika mahali wananchi wanazikatia tamaa hizo haki
zao kwani kuna baadhi wameshinda tangu 2015 lakini hawajawahi kufurahia huo
ushindi wao kutokana na kupigwa danadana,’’ alisema Colex.
Kwa upande wake Msajili wa hati Msaidizi, Mkoa wa Singida, Palmon Rwegoshora
alisema lengo lingine la kikao kazi hicho ni kuwahamasisha maafisa ardhi kwenda
kwa wananchi kuwaeleza gharama za umilikishaji zimepungua kutoka na punguzo
lililotolewa na Serikali ambalo ni nusu bei ya gharama za awali.
Alisema kutokana na punguzo hilo wanategemea watu wengi watamilikishwa
viwanja vyao na kupata hati na kwenda kwenye taasisi za kifedha kukopa na kwa
upande wa wizara itakuwa imeongeza wigo wa kukusanya kodi kwa kuwa kila mwaka
kwa mtu ambaye atakuwa amemilikishwa ardhi atakuwa akilipa kodi.
Mpima ardhi Mkoa wa Singida, Sesaria Williams ameungana na Serikali kwa
uamuzi iliochukua ya kutoa punguzo hilo ambapo awali maombi ya umilikishwaji yalikuwa
Sh.50,000 lakini sasa ni Sh.25 na ada ya ramani ndogo ya hati ilikuwa Sh. 20,000
lakini sasa ni bure na maombi ya kumilikishwa ilikuwa ni Sh.20,000 ambapo sasa
ni Sh.5000 jambo ambalo halijawahi kutokea tangu nchi hii ipate uhuru.
Mratibu wa Kodi ya Ardhi Mkoa wa Singida, Benedict Mombeki alisema kodi ya pango la ardhi mkoani hapa bado kuna muitikio mdogo zaidi au wananchi wanauchumi wa chini na wanailipa kwa kusuasua.
Alisema wamewazoea wale wanaolipa kodi kwa kila mwaka ambao wanalipa pesa
ndogo na kuwa wale wenye madeni makubwa wanashindwa kulipa pengine ni kutokana
na kuwa na madeni makubwa kutokana na kuwa na riba kubwa hivyo kuwawia vigumu
kuilipa.
Mwombeki alisema kodi hiyo ni wananchi, taasisi za Serikali, mashirika ya
umma pamoja na makampuni binafsi na kuwa ukiangalia kwa Mkoa wa Singida,
asilimia kubwa ya madeni yapo upande wa taasisi za Serikali, mashirika ya umma
na watu binafsi wachache ambao wanadaiwa kodi kwa muda mrefu.
‘’ Wengi wameshindwa kulipa kutokana na kuwa na madeni makubwa zaidi ambayo
walilimbikiza yakiwa na riba yake na kuwa tukiangalia mwaka wa fedha uliokwisha
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alitoa msamaha kwa wananchi , kampuni zote na
taasisi za Serikali kulipa kodi pasipo kulipa riba katika deni lao la msinghi..
Alisema kwa Mkoa wa Singida muitikio ulikuwa mdogo mno kwani waliolipa na
kuhorodheshwa walikuwa watu 73 na waliokuwa wakidaiwa kodi ya pango la ardhi ni
zaidi ya watu 20,000.
Alisema watu wengi walikosa fursa ya kulipa deni hilo licha ya kufika ofisi
za ardhi na kuchukua bili zao lakini
walishindwa kulipa na kuwa kutokana na huo msamaha kutakuwa na deni kubwa.
Alisema timu ya mkoa inaendelea kuwahamasisha na kuelimisha wananchi juu ya ulipaji wa kodi ya ardhi, madhara yake na wengine wanaendelea kuyapungu na kuwa uzuri wake hivi sasa imetengenezwa namba maalumu ya udhibiti ya kumsaidia mwananchi kulipa kidogo kidogo na kutokana na hatua hizo za wizara kunaweza kukawa na makusanyo makubwa mwaka huu au mwaka ujao wa fedha baada ya kurahisishiwa namna ya kuyakusanya.
Post a Comment