MEYA MTINIKA TEMEKE ATAKA KASI UFUATILIAJI ELIMU WATU WAZIMA
Na Shalua Mpanda-TMC
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam Abdallah Mtinika amewaagiza wakuu wa idara kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya shughuli za elimu ya watu wazima.
Ametoa maagizo hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kiwilaya kimefanyika leo Oktoba 09,2023 ambapo viongozi mbalimbali pamoja na baadhi ya wanafunzi kutoka shule za Msingi walihudhuria.
Pia Meya Mtinika amewataka wakuu hao wa Idara kuipa "uhai" elimu hiyo kwa kuhamasisha,kuanzisha,kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu ya watu wazima.
"Naomba wananchi wenzangu kuzitumia fursa mbalimbali za Elimu ya Watu Wazima na walio nje ya mfumo rasmi kuondoa changamoto za ujinga,umaskini na maradhi ambazo bado tunazo."
Kwa upande wake Ofisa Elimu ya Watu Wazima Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Donasiana Njuu amesema elimu nje ya mfumo rasmi inatoa fursa kwa watu kujiendeleza kutoka hatua ya chini kielimu hadi hatua za juu kupitia Programu zake mbalimbali .
Maadhimisho ya mwaka huu yenye kauli mbiu "Kukuza uwezo wa kusoma na kuandika kwa ulimwengu unaobadilika:Kujenga Misingi ya Jamii endelevu yenye amani",kitaifa yanafanyika katika mkoa wa Pwani.
Post a Comment