Header Ads

test

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAELIMISHA WANANCHI WIKI YA VIJANA BABATI

Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya
Muungano na Mazingira katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa
yanayofanyika Babati mkoani Manyara.

Maonesho hayo yanayokwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa
Uhuru 2023 yameanza Oktoba 8 na kutarajiwa kumalizika Oktoba 14,
2023.

Akitoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda hilo Afisa Elimu
Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Martha Ngalowera amesema
vijana wanaweza kujipatia kipato kwa kuangalia fursa mbalimbali za
utunzaji wa mazingira zinazopatikana katika eneo analoishi.

Bi. Martha amesema mazingira yanatoa fursa nyingi kwa vijana kama
vile upandaji wa miti wa matunda unavuna matunda na kujipatia fedha
lakini hata miti yenyewe ni biashara kubwa.

“Utunzaji wa taka unaweza ukazalisha mbolea ambapo inatumika na
watu wengi katika mashamba na watunza bustani hiyo yote ni biashara
ambayo kijana anaweza akafanya kujipatia kipato wakati huohuo
anatunza mazingira.

“Kwa mfano unapokusanya chupa, kuna viwanda ambavyo hutumia tena
hizo chupa kwa matumizi mbalimbali, hapo unaona kwamba unaweka
mazingira safi na pia kupata fedha kwa biashara hiyo,” amesema Bi.
Martha.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw.
Onespholy Kamukuru amesema lengo la uwepo wao katika ‘Wiki ya
Vijana’ ni kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
“Tumeandaa mada ambayo inaelezea nafasi ya vijana katika uhifadhi
wa mazingira, kikubwa tunaangalia shughuli ambazo vijana wanazifanya
kwaajili ya kuongeza kipato ikiwemo kuwa na shughuli za uhifadhi kama
vile ufugaji wa nyuki, utunzaji wa taka ambapo vijana wanaweza
wakaungana na kuwa kikundi na kujipatia kipato.

“Aidha tunatoa historia ya Muungano ambapo wanafunzi wamekuwa
wakinufaika wakubwa wa elimu hii ambayo naamini kuna baadhi ya vitu
wanajifunza shuleni na hapa tunawaongezea maarifa mengine hata yale
ambayo hawakuyapata huko.”

Mhandisi Kamukuru ameongeza katika uhifadhi wa mazingira
kumekuwa na fursa nyingi kwa vijana kwa kuandika maandiko na kupata
fedha ambapo wamekuwa wakisaidiwa kupata wafadhili kutokana na
maandiko yao ya miradi hasa yanayoendana na uhifadhi wa mazingira.

Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2023 yanafanyika Babati mkoani
Manyara ambapo ujumbe ni “Vijana na ujuzi rafiki wa mazingira kwa
maendeleo endelevu.”


Aidha, ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu 2023
unaohusu Mabadiliko ya Tabianchi Hifadhi Mazingira sambamba na
Utunzaji wa Vyanzo vya Maji “Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji
kwa Ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa.”







Afisa Elimu Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa
Rais Bi. Martha Ngalowera akitoa elimu ya Muungano na Mazingira kwa
wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika
maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani
Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14 ambapo inakwenda
sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.




Mhandisi Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa
Rais Bw. Onespholy Kamukuru akitoa elimu ya Muungano na Mazingira
kwa wanafunzi waliotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika
maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani
Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14, 2023 ambapo inakwenda
sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.

No comments