Header Ads

test

JUMLA YA TAASISI 802 ZAPATIWA MAFUNZO MATUMIZI YA NeST.

 

Na Mwandishi Wetu-Dodoma

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA inaendelea na hatua ya utoaji mafunzo kwa Taasisi za umma juu ya matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa kielektroniki NeST ambapo mpaka sasa jumla ya Taasisi 802 zimekwisha kupatiwa mafunzo.

Akizungumza Ofisini kwake leo, Mkurugenzi wa huduma za Ushauri na Kujenga Uwezo PPRA, Mhandisi Amin Mcharo amesema kuwa mafunzo kwa Watumishi wa Taasisi za Umma kuhusu matumizi ya mfumo wa NeST yanaendelea ambapo mpaka sasa jumla ya Washiriki 8435 kutoka Taasisi 802 wamepatiwa mafunzo.

“Mpaka juzi tarehe 28 Novemba 2023, tumekuwa na orodha ya jumla ya washiriki 8435 waliopatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo, washiriki hao ni wa kutoka katika Taasisi za Umma 802”  Alisema Mhandisi Mcharo

Amesema kuwa idadi hiyo  ni sawa na wastani wa robo tatu ya Taasisi zote zilizojisajili kwenye mfumo, ambapo jumla ya taasisi zotezilizojisajili mpaka sasa ni 1042.

Aidha amewataka wakuu wa Taasisi za Umma ambao Taasisi zao hazijapata mafunzo kupeleka watumishi wao PPRA kupata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kutumia mfumo wa NeST kwa ufanisi zaidi, kwani kupatiwa mafunzo na wawezeshaji kutoka nje ya PPRA kunaweza kupunguza ufanisi wa mafunzo hayo kutokana na baadhi ya wawezeshaji wa nje  kupotosha kwa kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST.

“Niwaombe Wakuu wa Taasisi za Umma kuwatumia wawezeshaji kutoka PPRA ili kuendesha mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo, kwani kutumia wawezeshaji wanaotoka nje ya PPRA kwa kiasi kikubwa kunahatarisha ufanisi wa mafunzo, kwa sababu baadhi ya wawezeshaji wa nje hawana uelewa wa kutosha juu ya matumizi sahihi ya mfumo wa NeST.” Aliongezea.

Pia alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji mafunzo hayo ni baadhi ya watumishi waliopendekezwa kushiriki mafunzo na Taasisi zao  kutofika mafunzoni au kufika nje ya wakati, suala linalozorotesha ufanisi wa mafunzo na hatimae kuzalisha watumiaji wa mfumo wasio na uelewa wa kutosha.

PPRA inaendelea kutoa mafunzo ya mfumo wa NeST katika vituo mbalimbali vilivyo chaguliwa ili kuhakikisha wadau wote muhimu wanautumia mfumo ipasavyo.



No comments