Header Ads

test

TANZANIA YATOA WITO KWA MATAIFA TAJIRI DUNIANI




SERIKALI imezitaka Jumuiya za Kimataifa zisaidie kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi wake.

“Tumeliomba jukwaa hili lione namna ya kushirikisha nchi zinazoendelea kuboresha uchumi wetu ndani ya nchi kwa kukuza biashara na milango ya uwekezaji na namna nyingine zinazoweza kusaidia kuinua uchumi wetu,” amesema.

Hayo yamesema leo (Ijumaa, Novemba 17, 2023) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha tamko la Serikali kwenye ufunguzi wa mkutano wa pili wa Jukwaa la Sauti za Nchi Zinazoendelea uliofanyika kwa njia ya mtandao chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa ameliomba jukwaa hilo liangalie namna linavyoweza kushirikisha uchumi wa dunia na kuufungamanisha na uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Akielezea kuhusu masuala mengine, Waziri Mkuu ameliomba jukwaa hilo lihakikishe linatafuta majibu ya changamoto za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, masuala ya nishati mbadala, uwezeshaji wa vijana na wanawake

Jukwaa hilo linaziwezesha nchi zinazoendelea kujadili changamoto zinazowakabili na kupaza sauti zao ili ziweze kuwasilishwa kwenye mkutano wa kundi la nchi 20 zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi (G20) utakaofanyika Novemba 20, mwaka huu.

Mapema, akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa India, Bw. Modi alisema licha ya kwamba jukwaa hilo lina wanachama zaidi ya 100, bado wote wanaunganishwa na mahitaji na vipaumbele ambavyo vinafanana.

“Desemba, mwaka jana, India ilichukua uenyekiti wa G20 lakini tukajipa jukumu la kuhakikisha sauti za nchi zinazoendelea zinasikika na ndiyo maana tukaandaa mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Sauti za Nchi Zinazoendelea (Voice of Global South Summit -VOGSS) ili tuweze kupaza sauti zetu kwa mataifa tajiri na mfano ni kuzindua umoja wa watumiaji wa nishati mbadala (Global Biofuel Alliance).”

Mkutano wa leo umeshirikisha wakuu wa nchi na wawakilishi 13 wakiwemo marais sita ambao ni Rais Sitiveni Ligamamada Rabuka (Fiji), Rais Joko Widodo (Indonesia), Rais Dkt. William Ruto (Kenya), Rais Sadyr Nurgojoevich Japarov (Jamhuri ya Kyrgyz), Rais Richard Ravalomanana (Madagascar) na Rais Daviv Adeang (Nauru).

Mawaziri Wakuu walioshiriki mkutano huo ni Bibi Sheikh Hasina wa Bangladesh, Dkt. Abiy Ahmed Ali (Ethiopia), Bw. Pravind K. Jugnauth (Mauritius), Bw. James Marape (Papua New Guinea), Bw. Ferdinand Marcos (Philippines) na Mshauri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Bhutan, Bw. Chogyal Dago Rigdzin.

No comments