WAKAZI WA KATA YA IKOMA WAPATIWA ELIMU KUHUSU UBORESHAJI WA MAJARIBIO
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanaendelea kushiriki vipindi vya redio katika redio za kijamii kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa wakazi wa kata ya Ikoma iliyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoa wa Mara. Elimu ya mpiga kura inatolewa kwa wakazi hao ili kuwawezesha kuzifahamu sheria, kanuni, miongozo, maelekezo na taratibu kuhusu uboreshaji wa majaribio unaoanza kesho Novemba 24,2023.
Akizungumza wakati wa kipindi cha Morning Sachita kilichorushwa leo na redio ya Sachita iliyopo Tarime Mkoa wa Mara, Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Elimu ya Mpiga Kura Bi. Monica Mnanka amewaeleza wakazi wa Kata ya Ikoma kuwa zoezi la kujiandikisha na kuboresha taarifa litaanza saa 2.00 Asubuhi hadi 12.00 kwa muda wa siku saba katika vituo sita vya kuandikisha wapiga kura vilivyopo katika kata hiyo. Amevitaja vituo hivyo vya uandikishaji kuwa ni Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Ikoma, shule ya Msingi ya Bugire, Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ikoma, Shule ya Msingi Kogaja , Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Nyamasanda na Shule ya Msingi Nyamasanda.
Bi. Mnanka aliambatana na Afisa Habari Mwandamizi Bw. Hussein Makame ambaye alielezea kuhusu wahusika wa zoezi la uboreshaji wa majaribio hayo. Wahusika hao ni pamoja na wanaoandikishwa kwa mara ya kwanza ambao ni raia wa Tanzania na wenye umri wa miaka 18 au watafikisha umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi wa mwaka 2025, wanaoboresha taarifa zao na kuondoa wale waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari. Mfano waliofariki dunia.
Pia, wakati akijibu swali la Msikilizaji, alifafanua kuwa Tume imeboresha mifumo yake ya uandikishaji wapiga kura na imeweka utaratibu unaowawezesha wapiga kura waliomo kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha na kuhamisha taarifa zao kwa njia ya mtandao. Wapiga kura hao wataingia kwenye Tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi www.nec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja na kubofya kiunganishi Boresha taarifa za mpiga kura na kufuata maelekezo au kutumia anuani ya ovrs.nec.go.tz na kuanzisha mchakato.
Akizungumzia mambo ambayo hayatakiwi kufanyika wakati wa uboreshaji wa majaribio, Bi. Mnanka amesema kuwa ni kosa la jinai mwananchi anyeandikishwa au mpiga kura anayeboresha kutoa taarifa za uongo. Amesisitiza kuwa watakaotoa taarifa za uongo au kujiandikisha zaidi ya mara moja watachukuliwa hatua za kisheria.
Uboreshaji wa majaribio unafanyika kwa ajili ya kupiga uwezo na ufanisi wa vifaa na mifumo ya uandikisha ambayo imeboreshwa ili kubaini iwapo kutajitokeza mapungufu ili yafanyiwe kazi kabla ya kuanza zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la wapigakura litakalohusisha nchi nzima.
Tume inatekeleza jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa mujibu wa kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.
Ushiriki wa watumishi wa Tume katika vipindi vya elimu ya mpiga kura ni mojawapo ya njia zinazotumika kutoa elimu hiyo. Awali katika kutoa elimu ya mpiga kura, Tume ilikutana na wadau wa uchaguzi waliowakilisha makundi mbalimbali katika jamiii kitaifa na ngazi ya mikoa tarehe 16,17 na 20 Novemba, 2023. Wawakilishi hao walikuwa ni Viongozi wa vyama vya siasa viongozi wa dini, wazee wa kimila na watu wenye ulemavu, wanawake, vijana, wahariri na waandishi wa habari.
Mkurugenzi Msaidizi Bi. Monica Mnanka akizungumza wakati wa kipindi cha Morning Sachita lilichorushwa kupitia redio Sachita iliyopo Wilaya ya Tarime leo Novemba 23, 2023. Kushoto ni Mtangazaji wa redio hiyo Bi.Stephania Jeremia.
Afisa Habari Mwandamizi Bw. Hussein Makame akizungumza wakati wa kipindi cha Morning Sachita lilichorushwa kupitia redio Sachita iliyopo Wilaya ya Tarime leo Novemba 23, 2023.
Post a Comment