Header Ads

test

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NA BIASHARA ILI KUKUZA UCHUMI NA MAENDELEO YA WANANCHI

Na. Joseph Mahumi, WF, Morogoro


Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanyia biashara ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa kukuza ajira na vipato vya wananchi kupitia uwezeshaji wa sekta mbalimbali za uzalishaji mali.

Hayo yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), wakati akifungua Kongamano la Wahariri wa vyombo vya Habari nchini lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, mkoani Morogoro.

CPA Mkude alisema kuwa, Shughuli za uchumi nchini zimeendelea kuimarika licha ya kukabiliana na changamoto zilizotokana na utekelezaji wa sera ya fedha ya kupunguza ukwasi katika nchi zilizoendelea, migogoro ya kikanda na kimataifa, kuongezeka kwa bei za bidhaa za petroli, gharama kubwa za mikopo na mabadiliko ya tabianchi. 

Alisema kuwa, Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022. Ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kilimo, ujenzi na uchimbaji madini.

“Viashiria vya uchumi kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2024 vinaonesha uchumi kuendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya awamu ya sita za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na kuimarisha sekta za uzalishaji na huduma za jamii. 

Alisema kuwa kufuatia jitihada hizo, Pato halisi la Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024 lilikua kwa wastani wa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023” alisema CPA Mkude.

Aliongeza kuwa, Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.8 mwaka 2025 na asilimia 6.1 mwaka 2026. Ukuaji huu utategemea utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati inayohusisha miundombinu ya nishati na usafirishaji, kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili - ASDP II, utekelezaji wa mapendekezo na Mkakati wa Tume ya Haki Jinai, uwepo wa utawala bora pamoja na uwekezaji wa Serikali katika sekta za huduma za jamii.

“Tunamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa miongozo, mipango na maelekezo yake thabiti anayotupatia katika kusimamia uchumi wa nchi. Kutokana na umahiri wake katika uongozi, na kusimamia kwa dhati diplomasia ya uchumi, wadau mbalimbali, zikiwemo Taasisi kubwa za Fedha Duniani, ikiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB na wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani waliko hapa nchini, wamekuwa wakiimwagia sifa Tanzania kwa mafanikio makubwa ya kusimamia uchumi na sera zake za fedha na Bajeti” aliongeza CPA Mkude.

CPA Mkude, alitumia fursa hiyo pia kuwataarifu wahariri hao kuwa, Tanzania imepata fursa na bahati kubwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu wakuu wa Serikali wa Afrika - African Association of Accountants Generals (AAAGs) ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 5 Disemba, mwaka 2024 jijini Arusha; katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), na kufunguliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa Mkutano huo unaotarajiwa kuwa na washiriki wapatao 2000 kutoka nchi 57 wanachama za Umoja wa Afrika, una lenga Kujenga Imani ya Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu (Building Public Trust in PFM Systems for Sustainable Growth). Pamoja na kuwakutanisha wahasibu wote Tanzania, pamoja na kada zenye uhusiano wa karibu na uhasibu kama; Wakaguzi wa hesabu, Maafisa ugavi na Maafisa TEHAMA ili kuweza kujenga misingi bora ya Usimamizi wa Fedha na mali za Umma.

“Wizara ya Fedha imebaini kuwa mkutano huu ni muhimu katika kukuza utalii wa Mikutano na Matukio (MICE Tourism) pamoja na kutangaza utalii kimataifa. Tunaamini Washiriki watakaotembelea hifadhi hizi watavitangaza vivutio vyetu katika nchi zao” alisema CPA Mkude.

Aliongeza kuwa Washiriki wote wanatakiwa kujisajili kupitia lango (portal) ya https://conference.aaag.org.zm kuanzia sasa hadi tarehe 01 Desemba, 2024 na ada ya ushiriki ilipwe kupitia Akaunti Namba 99924915301 iliyopo Benki Kuu ya Tanzania yenye jina African Association of Accountants General (AAAG).

Pamoja na Hayo aliwashukuru wahariri hao na kuwahakikishia kuwa Wizara ya fedha inatambua umuhimu na mchango wao mkubwa katika kufikisha taarifa za Serikali kwa umma, hivyo kuchangia ufanisi wa utekelezaji wa Mkakati wetu wa Mawasiliano kwa Umma na vilevile maendeleo ya Watanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kifedha.

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wakifuatilia hotuba ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude (Hayupo pichani), wakati akifungua Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, mkoani Morogoro, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ambapo alitumia fursa hiyo pia kuwataarifu wahariri hao kuwa, Tanzania imepata fursa ya kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali wa Afrika - African Association of Accountants Generals (AAAGs) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 5 Disemba, mwaka 2024 jijini Arusha; katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), na kufunguliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, akizungumza wakati akimkaribisha Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude (Hayupo pichani) kufungua Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, mkoani Morogoro, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ambapo aliwapongeza Wahariri hao kwa kuendeleza ushirikiano thabiti na Wizara katika kuhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayojiri.
Mwenyekiti wa Wahariri wa Vyombo vya Habari wa Kongamano lilioandaliwa na Wizara ya Fedha, Bw. Ben Mwang'onda, akizungumza jambo wakati wa Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, ambapo aliwashukuru kwa ushirikiano wao katika kuhabarisha Umma hususan masuala ya Fedha na taarifa mbalimbali zinazochagiza ukuaji wa uchumi wa nchi na kuifanya Tanzania iwe kinara katika Usimamizi na ukuaji wa uchumi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mkuu wa Kitengo cha Pensheni, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Babu Kiguhe, akifafanua jambo kuhusu aina ya mafao ya pensheni yanayolipwa na Wizara ya Fedha, wakati wa Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, mkoani Morogoro, ambapo pamoja na mambo mengine amewasisitiza wahariri hao kuhabarisha umma kuhusu huduma kutolewa bila malipo ili kusaidia wastaafu kukwepa matapeli.
Afisa Hesabu Mkuu  Idara ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Erasto Kivuyo, akitoa mada kuhusu Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2025/2026 na namna Bajeti ya Serikali inavyoandaliwa, wakati wa Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, mkoani Morogoro.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude (Katikati walioketi), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja (kushoro), na Mwenyekiti wa Wahariri wa Vyombo vya Habari wa Kongamano lilioandaliwa na Wizara ya Fedha, Bw. Ben Mwang'onda (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Wahariri wa vyombo vya Habari nchini baada ya kumalizika kwa Kongamano la Wahariri hao lililoandaliwa na Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa Mikutano wa  8.8, Mkoani Morogoro.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)




No comments