Serikali Yatilia Mkazo Ushirikiano wa Wadau Kukuza Sayansi na Teknolojia
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amesema kuwa Serikali itaendeleza msimamo thabiti wa kujenga mazingira wezeshi kwa sayansi, teknolojia na ubunifu wa vijana.
Akizungumza leo Dar es Salaam kwa niaba ya Profesa Nombo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa, wakati wa Maonesho ya 15 ya Kitaifa ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira hayo wezeshi kwani ndio msingi muhimu kwa vijana kuwa na ujuzi
Amesema Programu kama YST ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanajengewa ujuzi na mitazamo itakayoliendesha taifa kuelekea maendeleo kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya 2050.
Amesisitiza kuwa Serikali inabaki na dhamira ya dhati ya kujenga mazingira yenye nguvu ya kustawisha sayansi, teknolojia na ubunifu,” amesema Prof. Kihampa na kuongeza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, mpango wa YST umekuwa jukwaa la kitaifa la kukuza hamu ya kisayansi miongoni mwa wanafunzi wa sekondari.
Ameongeza kuwa hatua ambayo imeondoa dhana potofu kwamba masomo ya sayansi ni magumu. YST imejikita sambamba na sera za kitaifa za elimu na mafunzo, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
“Hususani SDG 4 (Elimu Bora), SDG 9 (Viwanda, Ubunifu na Miundombinu) na SDG 17 (Ushirikiano kwa Malengo). Kwa mwaka huu pekee, mradi huo umefikia zaidi ya wanafunzi 14,000 na walimu 3,000,”amesema Prof. Kihampa
Awali Mwenyekiti wa YST, Profesa Yunus Mgaya amesema maonesho ya mwaka huu yamevutia wanafunzi 3,085 na walimu 1,489, yakitoa jukwaa hai la ubunifu na mijadala ya kisayansi.
“Safari hii, iliyoanza na shule chache pekee katika mikoa mitatu, sasa imekua na kufikia harakati za kitaifa, jambo tunalojivunia. Miradi ya mwaka huu imelenga suluhu kwa changamoto za taifa katika kilimo, sayansi ya mazingira, teknolojia, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya kijamii,” amesema.

“Miradi 237 iliwasilishwa mwaka 2024, na kati yake miradi 45 imechaguliwa kuonyeshwa mwaka huu. Miradi hii inalenga kutoa suluhisho la vitendo kwenye usalama wa usafirishaji, mifumo ya kidijitali, kupunguza ajali za bodaboda, kudhibiti foleni, usalama wa chakula, afya, nishati mbadala, uhifadhi wa mazingira na changamoto nyingine za kijamii.”
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wadau, wakiwemo wawekezaji wa viwanda, kushirikiana na serikali kuwekeza katika sayansi na ubunifu ili kuongeza uzalishaji na kuendeleza wataalamu wa ndani.
Pamoja na hayo amewatia moyo wanafunzi walioshiriki bila kushinda, akisema kushiriki pekee ni ushindi mkubwa.”Katika zaidi ya waombaji 50,000, ninyi mmechaguliwa. Ni fahari ya taifa letu. Ubunifu wenu ni uthibitisho mustakabali wa maendeleo ya kisayansi ya Tanzania ni angavu,” amesema.
Wakati huo huo Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Caren Rowland, ameeleza athari za mpango huo zimekuwa dhahiri kwa sababu kupitia msaada wake kwa kushirikiana wadau wengi ikiwemo RAD Foundation zaidi ya wanafunzi 53 ambao ni washindi wa YST wamepata ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu.
Pia mafunzo ya walimu yakiendelea kuwa nguzo kuu ya mpango huu kwa lengo la kukuza elimu ya sayansi ya vitendo.Taasisi hiyo imekuwa mfadhili mkuu wa YST kwa takribani miaka 15.
Post a Comment