BENKI YA DCB YAMTAMBULISHA MKURUGENZI MTENDAJI WAKE MPYA
Benki ya Biashara ya DCB, moja kati ya benki kongwe inayoongoza katika mabenki yenye ukubwa wa kati, imemtambulisha Mkurugenzi Mtendaji wake mpya katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alimtambulisha Bwana Sabasaba Moshingi, kuchukua nafasi hiyo adhimu ya kushika usukukani wa kuongoza benki hiyo akisema, licha ya mchakato kuchukua muda mrefu lakini kama benki pamoja na wanahisa wake wanayo furaha kwa kumtapata mtu anayekidhi vigezo walivyohitaji.
“Benki yetu, wateja wetu pamoja na wanahisa wake walihitaji mtu sahihi atakayesukuma mbele vyema gurudumu la maendeleo la DCB, kwa weledi, umakini na uhakika zaidi, atakayeweza kuitoa DCB mahali ilipo na kuipeleka mbele zaidi kimafanikio, na baada ya kupitia hatua na taratibu kadhaa Bodi na Menejimenti ya DCB zina kila sababu ya kutembea vifua mbele kwa kumpata mtu sahihi ambaye kutokana na ukongwe wake katika tasnia za kibenki na taasisi za fedha tuna imani matarajio yetu yametimia.
“Bwana Mshingi ni Mtaalamu mbobevu katika masuala ya benki kwa zaidi ya miaka 12, Bwana. Moshingi, analeta pamoja naye hazina kubwa ya uzoefu katika tasnia za kibenki za Kitaifa na Kimataifa akiwa na rekodi thabiti katika Uendeshaji wa Benki, Biashara za Fedha, Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi, Masuala ya Mikopo na mengineyo.
“Bwana Moshingi ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara katika Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amethibitishwa na Taasisi ya Mabenki Tanzania na kabla ya uteuzi wake wa sasa, Bw. Moshingi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB akishika pia nafasi mbalimbali za uongozi katika benki za, Standard Chartered, Stanbic na KCB.
“Ni matumaini ya benki yetu, wateja wetu na wanahisa wetu kuwa ujio wa Bwana Moshingi umekuja kwa wakati sahihi na kutokana na historia iliyotukuka ya mafanikio aliyoyapata katika taasisi alizowahi kufanya kazi, tunaiona benki yetu ikizidi kupanda kila siku kuelekea katika kilele cha mafanikio”, alisema Bi Zawadia.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya benki, Bi Zawadia alisema DCB inazidi kupiga hatua siku hadi siku ikizidi kuendeleza jukumu mama la kuanzishwa kwake tokea miaka 21 iliyopita likiwa ni kutoa huduma bora za kifedha ikijikita zaidi katika kusaidia miradi endelevu ya kupunguza umasikini na kuendeleza jamii kwa kutoa huduma na bidhaa zenye ubunifu kwa wateja.
Alisema Benki ya DCB kwa miaka 21 imepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo ikikuza mtaji wake kutoka kiasi cha shs Bilioni 1.7 ilipoanzishwa hadi kufikia kiasi cha shs Bilioni 27.5 kwa sasa, maendeleo hayo yalichangia mabadiliko mbalimbali katika benki ikiwa ni pamoja na kutoka kuwa Benki ya Kijamii hadi kuwa Benki kamili ya Biashara.
“Benki yetu imeendelea kunyanyua wajasiriamali wengi wadogo kiuchumi ambao hawakuwa na namna ya kupata mitaji huku DCB ikiwa mstari wa mbele katika kutoa mikopo ikiwemo mikopo ya vikundi kwa wajasiriamali wadogo, mikopo ya biashara kwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa.
“Benki yetu imeendelea kupata faida mwaka hadi mwaka, kwa mwaka jana benki ilipata faida baada ya kodi ya shs 747 milioni, faida iliyochangiwa na mapato yasiyotokana riba ya shs 10.3 bilioni ambayo ni mafanikio ya asilimia 111 ya malengo tuliyojiwekea kwa mwaka 2022, huku mapato yatokanayo na riba yakifika shs 28.6 bilioni ikiwa ni asilimia 86 ya malengo tuliyojiwekea.
Akizungumza zaidi Bi Zawadia alisema “mali za benki zimekuwa hadi kufikia shs 227 bilioni hadi kufikia Septemba mwaka huu, kutoka shs 132 bilioni kwa mwaka 2018. Tukijivunia ukuaji huu ulioitoa benki yetu kutoka kwenye kundi la benki ndogo za biashara hadi kufikia benki za ukubwa wa kati nchini. Haya ni mafanikio makubwa ambayo ni matumaini yetu Mkurugenzi Mtendaji wetu mpya Bwana Sabasaba Moshingi ataendelea kushika usukani wa DCB kwa ustadi mkubwa kwa ukuaji zaidi wa benki yetu.
“Benki ya DCB itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wa maeneo ambayo hakuna matawi ya benki wanafikia na huduma za kifedha, ikienda sambamba na vipaumbele vya benki yetu kuhakikisha huduma zetu bora za kibenki zinapatikana nchi nzima na hii inatikana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika huduma zetu za kibenki kwa njia za kidigitali, hususan DCB Wakala na DCB Kidigitali inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki mahali walipo ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti.
“Huduma mbalimbali za kibenki zinapatikana kwa njia ya kidigitali mfano DCB Pesa ambayo mteja anaweza kufanya malipo na manunuzi kama vile, kuweka akiba au kutoa pesa, kulipa bili ya maji au umeme, kulipia ving’amuzi na pia kufanya malipo malipo ya serikali.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Bodi alitaja baadhi ya huduma na akaunti zinazoendesha na benki hiyo kama kaunti ya elimu ya DCB Skonga, Wahi Akaunti kwa wenye mahitaji ya kutimiza malengo kwa njia ya kuwekeza kidogo kidogo, Akaunti za Mshahara & mikopo ya nusu mshahara, akaunti ya Wastaafu, Mikopo ya Nyumba, Lamba Kwanza na nyinginezo nyingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo, Bwana Sabasaba Moshingi alitoa shukurani zake kwa Bodi ya Wakurugenzi na Wanahisa wa benki hiyo kwa kuwa na imani naye akiahidi kutumia uzoefu wake wa miaka 21 alioupata katika kutumikia taasisi mbalimbali za fedha kuiinua DCB kutoka mahali ilipo na kuipeleka mbali zaidi.
Alisema anajua matarajio ya wateja wa DCB, wanahisa wao, Bodi, wafanyakazi, wateja pamoja na wadau, ni matumaini yake kuwa kwa kutumia uzoefu alionao pamoja na ushirikiano wa wadau wote wataweza kutimiza matarajio makuu ikiwa ni kutoa huduma bora za kifedha zinazolingana na mahitaji ya wateja na kutoa huduma bora zenye kiwango cha kimataifa.
“Nikiwa na uzoefu wa miaka mingi katika maeneo ya biashara za kifedha, mikopo na wateja binafsi, ni matumaini yangu kuwa kwa pamoja tutaendeleleza azma hii kwa kutoa suluhu nyingi zaidi za mitaji kwa wafanyabiasha wadogo na wakati na pia kuliangalia kwa jicho la pembeni uboreshaji wa huduma za kifedha kwa njia za kidigitali ili zilingane na mahitaji ya watanzania lakini pia ziwe na ubora wa kimataifa.
“Nina imani kwa ushirikiano wa pamoja hakuna kitakachoshindikana, maendeleo niliyoyapata katika taasisi nilikotoka, yanawezekana na hapa pia, tukae tayari kwa biashara.
“Ndugu Mwenyekiti wa Bodi na Waandishi wa Habari, Kwa kuwa leo sio siku yangu, ni siku ya Mwenyekiti wetu, ni siku tu ya kutambulishwa kwangu, ningeomba niishie hapa ili panapo majaliwa ya Mungu basi tutawaita tena ili tuweze kuzungumza pamoja kuhusu maendeleo ya benki yetu ukizingatia kuwa wengi kati yenu tunafahamiana vizuri tokea huko nyuma”, alisema Bwana Moshingi.Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro (wa pili kulia), akimkabidhi nyaraka muhimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo, Bwana Sabasaba Moshingi, ikiwa ni ishara ya makabidhiano rasmi ofisi, wakati akimtambulisha kwa waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo. Wengine kushoto ni Katibu wa Benki, Bi. Regina Mduma na kutoka kulia ni, Ofisa Fedha Mkuu, Deusdedit Mulindwa na Mkurugenzi wa Biashara, Bi. Lilian Mtali.
Post a Comment